Kocha wa timu ya Tabora United raia wa Serbia Goran Kopunovic ameelekeza lawama zake kwa Uwanja wao wa nyumbani Ali Hassan Mwinyi kuwa na nyasi ndefu sana na kuzuia timu yake kucheza vizuri.
Nyasi zilikuwa ndefu kuliko kawaida na kufanya vijana wangu washindwe kucheza vizuri huku pia uwanja ukionekana kuwa na utelezi. Nilijaribu kuwaambia viongozi kuwa sijaridhika na urefu wa nyasi hizi lakini pengine hawakuzingatia na ndio hivyo yametokea matokeo hayo.
Aidha katika hatua nyingine hakusita kuzungumzia pia kukosekana kwa wachezaji wake muhimu kwenye kikosi cha leo.
Nimemkosa Paulin, Nimemkosa Banza ni wachezaji wangu muhimu sana japo wapo wengine waliojitahidi kucheza vizuri sana licha ya kutokuwa chaguo la kwanza. Kuna wachezaji wangu wapya nilitamani kuwatumia lakini niliambiwa haiwezekani kuna vitu havijakaa sawa bado, sasa hata sielewi nini kinaendelea.
Licha ya kusikitishwa na matokeo haya ya kufungwa mabao mengi lakini hakuacha kuwasifia Simba na hasa ubora wao.
Kiukweli inaumiza. Bao 4 ni nyingi sana hasa ukiwa nyumbani lakini lazima tukubaliane kuwa Simba ni Simba tu ni timu ya daraja kubwa na uwezo wao ni mkubwa na leo wamecheza vizuri wakituadhibu kwenye makosa yetu. Nawapongeza pia.
Goran Kopunovic ameambulia kipigo cha 2 mfululizo NBC baada ya kufungwa 1-0 na Yanga kwenye mchezo wao uliochezwa Jamhuri Dodoma.
Wakiwa wamevuna alama 15 tu kwenye mechi zao 14 wakishinda mechi 3 tu na kutoa sare mechi 6, Tabora United hawapo kwenye nafasi nzuri wakiwa kwenye 10 la 2 kwenye msimamo wa Ligi Kuu.