Connect with us

NBC Premier League

AHMED: TUMEJIANDAA KUSHINDA KESHO.

Klabu ya Simba inatarajia kushuka dimbani hapo kesho kuikabili klabu ya Azam kwenye uwanja wa CCM Kirumba, Jijini Mwanza katika mwendelezo wa michezo ya Ligi kuu kandanda Tanzania Bara.

Mchezo huo utapigwa saa kumi [10:00] jioni na Simba ndio mwenyeji wa mchezo huo, kuelekea mchezo huo hapo kesho Afisa habari na mawasiliano wa klabu ya Simba Ahmed Ally ameweka wazi kuwa maandalizi yao ni ya kupata matokeo mbele ya Azam.

““Tumeleta mechi Mwanza kwa kutambua umuhimu na thamani yenu. Tunajua nguvu yenu hakuna linaloshindikana. Tumejiandaa vizuri kupata matokeo lakini haitakuwa rahisi tukiwa peke yetu, lazima Wanasimba tushikamane, tuungane tukapate matokeo kwa pamoja.”- Ahmed Ally akiongea na Wanasimba wa Kona ya Kayenze, Mwanza.

Kwa upande mwingine pia Afisa habari Ahmed Ally ameweka wazi kuwa klabu yao imepanda kwenye upande wa kiwango kwasasa tofauti na klabu zingine.

“Wanasimba wa Mwanza mna bahati sana ya kwenda kuiona Simba ikiwa ya moto. Wakati wengine wameshuka, Simba tumepanda. Wakati wao wanaumaliza mwendo, pumzi ya Mnyama imejaa. Simba imekuja ikiwa ya moto kwelikweli, Simba hii haina presha.”- Ahmed Ally aliongeza.

Huu ni mchezo wa kiporo ambao ulitakiwa kufanyika mwezi December mwaka jana, hata hivyo Azam inashika nafasi ya pili ya msimamo wa Ligi kama Simba itashinda basi itaiondosha Azam kwenye nafasi hiyo.

Simba inakimbizana na kinara klabu ya Yanga ambaye hadi hivi sasa imeizidi takribani alama tano na leo Yanga ina kibarua mbele ya Mashujaa ya Kigoma huku mashabiki wa Simba wakiiombea mabaya klabu ya Yanga.

Makala Nyingine

More in NBC Premier League