Connect with us

Michezo Mingine

NDOTO ZA TANZANIA KUCHEZA FUTSAL AFCON 2024 ZAZIMWA

Ndoto za timu ya Taifa ya Tanzania ya mchezo wa FUTSAL kufuzu kucheza AFCON 2024 Ya mchezo huo huko nchini Morocco zimezimwa hii ya leo baada ya kuondoshwa na Namibia kwa jumla ya mabao 8-8 kwenye mabao ya jumla baada ya kukubali kichapo cha mabao 6-3 hii leo.

Tanzania walitangulia kupata goli dakika ya 14 ya mchezo kabla ya Namibia kusawazisha kupitia shambulio lililojengwa vizuri baada ya walinzi wa Tanzania kuzubaa dakika ya 15.

David Gaspar aliwapatia Tanzania bao la 2 dakika 1 tu baadae baada kugongeana vizuri na Adam Ibrahim na kuifanya Tanzania kuwa mbele kwa mabao 2-1.

Namibia walisawazisha bao hilo dakika ya 17 ya mchezo kupitia pigo la adhabu lililopigwa kiustadi kwa shuti kali baada ya Tanzania kufikisha faulo zaidi ya 5 na muamuzi kuamuru pigo hilo.

Dakika ya 18 wakati Tanzania wakijiuliza wamepigwa na nini, Namibia Walijipatia bao la 3 kupitia kugongeana vizuri tena kwenye eneo la hatari la Tanzania na kisha kupigwa shuti kali lililomshinda golikipa Derrick Charles. Tanzania 2-3.

Mpaka Mapumziko, Tanzania walikuwa nyuma kwa mabao 3-2.

Kipindi cha pili Tanzania walirejea kwa kasi kujaribu kusawazisha huku Jamal Ally akioneka kuwa mwiba mchungu lakini golikipa wa Namibia alikuwa imara sana kuokoa michomo.

Dakika ya 26, Namibia walijibu mashambulizi kwa kasi huku wakionekana kuelewana vema zaidi hasa eneo la ushambuliaji na walifanikiwa kuandika bao la 4.

Dakika ya 27, Namibia walifanya tena shambulizi jingine la hatari wakiwakuta walinzi wa Tanzania wamezubaa na kupachika bao la 5 na kufanya ubao kusomeka Tanzania 2-5 Namibia.

Wakionekana kutepeta huku wasijue la kufanya, Tanzania wakajikuta wanazidi kuwa nyuma baada ya kuruhusu bao la 6 dakika ya 31. Tanzania 2-6 Namibia, 7-8 kwenye mabao ya jumla.

Isihaka Mwinyi alipokea pasi nzuri kutoka kwa Jamal Ally na yeye hakufanya ajizi na kuiandikia Tanzania bao la 3 na kufanya matokeo kusomeka 3-6 dakia ya 38 ya mchezo.

Dakika zote 40 zikatamatika kwa Namibia kushinda kwa mabao 6-3 huku kwa mabao ya jumla ikiwa mabao 8-8.

Kikanuni, Namibia wakafuzu kutokana na wao kufunga mabao mengi ugenini (6) kuliko walivyofunga Tanzania ugenini (5) na kuzima ndoto za Tanzania kucheza AFCON yao ya kwanza FUTSAL.

Makala Nyingine

More in Michezo Mingine