Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza ndio umeteuliwa na Simba SC kuwa uwanja utakaohodhi mtanange huu wa kukata na shoka ukiwahusisha Vigogo hawa wa soka nchini, Simba V Azam FC, mchezo unaotarajiwa kupigwa majira ya Saa 10 Jioni ya Leo.
Kama kuna nyakati ambayo Simba SC wanajihisi wako tayari zaidi kuwakabili Azam basi ni kipindi hiki wakiwa wameshika kasi baada ya kushinda Mechi 2 mfululizo tena bila kuruhusu bao lolote (1-0 v Mashujaa, 4-0 v Tabora United) wakiwa ugenini.
Ikiwa imefanya sajili za wachezaji wasiopungua watano(5) na wote wakionekana kuingia kwenye mfumo mapema zaidi na kuwa wenye msaada kwenye kikosi cha Wekundu hawa wa Msimbazi, Benchikha akifaidi matunda ya sajili zake na kuelekea mchezo huu atatamani kuvuna alama 3 zingine ili aweze kujiweka pazuri kwenye mbio za ubingwa.
Ushindi katika mchezo wa leo utwafanya wawe wamekusanya alama 9 zitakazowasogeza karibu na vinara wa ligi hiyo, Yanga ambao wana alama 8(37) zaidi yao lakini itawafanya wawashushe Wapinzani wao wa Leo, Azam FC wanaoshika nafasi ya 2 wakiwa na alama 31.
Tangu wapoteze kwa mabao 3-1 dhidi ya Namungo kwenye dimba lao la Azam Complex, Azam FC wanajivunia kwenda mechi 6 mfululizo bila kupoteza mchezo wowote wala sare wakivuna rekodi alama 18 na kuwaweka kwenye nafasi nzuri kwenye mbio zao za kuwania ubingwa.
Ushindi wa 4-0 dhidi ya Kagera Sugar ndio ushindi wao wa mwisho wa Ligi Kuu kabla haijaenda mapumziko huku pia wakionyesha kandanda safi na wakicheza Kibingwa, Youssouf Dabo na Bruno Ferry wanaingia kumenyana na Simba wakiwa na hali ya kujiamini kwa kiwango cha juu.
Wakiwa na alama zao 31, 6 nyuma ya Vinara Yanga, wanafahamu ushindi kwenye mchezo wa leo utawafanya wawe alama 3 tu nyuma yao lakini pia kutanua wigo wa alama kati yao na Simba mpaka alama 5 licha ya kwamba wana mchezo mmoja(1) mkononi.
Mambo ni mengi yaliyo mezani kwenye mchezo wa leo, sio tu kusaka alama 3 pekee bali pia kusaka Heshima ya Mzizima Derby. Hii ni zaidi ya mechi iliyojaa pia visasi vya hapa na pale, na wana Mwanza wanapata bahati ya kufaidi burudani hii.
WA KUTIZAMWA
Saido Ntibazonkiza Upande wa Simba amehusika kwenye mabao 6 mpaka hivi sasa kwenye michezo 12 aliyocheza, akifunga mabao 5 na kusaidia goli 1.
Feisal Salum amehusika kwenye mabao 12 kwenye mechi 13 alizocheza. Mabao yake 8 na pasi za usaidizi 4, ni mchezaji wa kuchungwa zaidi kwenye timu ya Azam.
DONDOO KUU
Katika Michezo 17 iliyowakutanisha miamba hawa ni mechi 3 pekee ndio zimemalizika bila goli hata 1. Upatikanaji wa Goli au zaidi ni asilimia 90 (90%).