Nyota wa timu ya Taifa ya Tanzania na klabu ya PAOK ya nchini Ugiriki Mbwana Ally Samatta amesema sababu kubwa ya yeye kufika alipo na kucheza Ligi kubwa Duniani ni maneno ya aliyekuwa Rais wa awamu ya nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.
Samatta kipindi akiwa anaitumikia TP Mazembe ya nchini Congo DR alitembelewa na Mh. Dkt. Jakaya Kikwete na kuambiwa kuwa Watanzania wanapenda kuwaona yeye na Thomas Ulimwengu wakifanikiwa zaidi.
“Jakaya Kikwete alitutembelea kambini tukiwa TP Mazembe mimi na Thomas Ulimwengu akatuambia Tunapenda tuwaone siku moja mkiwa Ulaya na mkipata mafanikio zaidi”.
“Kauli hiyo ya Rais ilituongezea nguvu ya kupambana mimi na Thomas, na nikaona kumbe hapa [TP Mazembe] sio mafanikio zaidi napaswa kupata mafanikio zaidi”, alisema Samatta.
Baada ya maongezi na Rais wa wakati huo Dkt. Jakaya Kikwete, Samatta aliongeza juhudi zaidi na hatimae kuibuka mchezaji bora wa ndani Afrika na mfungaji bora Afrika.
Akiwa kwenye kiwango bora alijiunga na KRC Genk ambapo aliendelea kuuwasha moto jambo ambalo liliwashawishi Aston Villa wamsajili, Samatta ameweka wazi kuwa siku amepokea ofa alitamani kujirusha dirishani kwasababu ya furaha aliyokuwa nayo.
“Nilipoambiwa kuna ofa ya Aston Villa nilitamani kujitupa dirishani kwasababu sikutarajia, nilikuwa kama chizi.”
Samatta ameeleza changamoto aliyokutana nayo wakati amejiunga na klabu ya Aston Villa ni janga la Corona na nafasi mbaya ambayo klabu ilikuwepo jambo ambalo lilibadili aina ya uchezaji wa timu na hivyo kupelekea yeye kutokufanya vizuri kama mwanzao.
“Sikukosea kwenda Aston Villa, wakati naingia nilianza vizuri, mfumo wa uchezaji ulibadilika baada ya Corona, walitaka kujilinda zaidi kuliko kushambulia kitu ambacho ni kigumu kwa mshambuliaji”.
“Hii ilikuja baada ya timu kuwa kwenye nafasi mbaya kwenye msimamo wa Ligi, ndio maana ukiangalia mechi nyingi tumetoa sare au tumeshinda goli moja”, Alisema Samatta.