Connect with us

NBC Premier League

SIMBA YAJINASUA KWENYE MTEGO GEITA GOLD

Simba wamevuna alama zote 3 kwenye mchezo wa ligi kuu Tanzania Bara baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Geita Gold kwenye mechi iliyokuwa na upambanaji wa kutosha ndani yake na kuifanya Simba kusogea mpaka nafasi ya 2 baada ya kufikisha alama 33, 7 nyuma ya Vinara wa ligi hiyo Yanga.

Simba walianza mashambulizi mapema na dakika ya 2 tu ya mchezo walipata kona, almanusura izae bao baada ya Kichwa cha Kibu Denis akiunganisha Kona ya Clatous Chama kiliokolewa kwenye mstari na Mwaita Gereza kabla ya Sadio Kanoute kupaisha mpira rejea.

Dakika ya 8, Chama alichonga vizuri mpira wa pigo huru lililotua kichwani kwa Sadio Kanoute ambaye alikuwa akicheza kama namba 10 hii leo nyuma ya Pa Omar Jobe lakini mpira ukaenda nje kidogo ya lango.

Simba walionekana kufeli kwenye mpango wao wa kuwa na viungo wengi wa kucheza ili kuifungua safu ya Ulinzi ya Geita Gold ambayo ilikuwa imara sana hii leo kwenye kuzuia na kucheza kinidhamu huku wakitumia kushambulia kwa kushtukiza kupitia kwa Edmund John, Offen Chikola na Jonathan Ulaya.

Licha ya kuumiliki mchezo lakini bado nafasi za wazi zilikuwa chache kwa Simba kipindi cha Kwanza. Mashambulizi ya hatari yakiwa ni machache sana ya kumsumbua golikipa Constantino.

Kipindi cha kwanza kilitamatika kwa suluhu ya 0-0.

Simba walimtambulisha Saidoo Ntibazonkiza nafasi ya Mzamiru Yassin huku Geita Gold wakiwatambulisha Saadun Nassor pamoja na Tariq Seif Kiakala na Erick Mwijage nafasi za Edmund John, Ramadhan Rashid na Offen Chikola wote wakidhamiria kuufungua mchezo kupata matokeo kipindi cha pili.

Licha ya Geita Gold kufanya mabadiliko kwenye safu yao ya ushambuliaji lakini hapakuwa na mashambulizi ya maana waliyoyafanya huku mpaka dakika ya 65 ya mchezo hawakufanya hata shambulizi 1 la hatari.

Simba waliwatambulisha mchezoni Luis Miquissone, Babacar Saŕr na Freddy Kouablan nafasi za Clatous Chama, Sadio Kanoute na Pa Omar Jobe huku Geita Gold wakimtambulisha Yusuf Dunia nafasi ya Jonathan Ulaya.

Dakika ya 69 Freddy Kouablan alijitengenezea nafasi na kupiga shuti kali lililowababatiza walinzi na mpira kuwa kona, hata hivyo kona hiyo haikuzaa matunda.

Geita Gold waliendelea kucheza chini kwenye eneo lao wakiamua kubaki na mpango wao kushambulia kwa kushitukiza kupitia Nassor Saadun, Erick Mwijage na Tariq Seif safari hii.

Dakika ya 81, Babacar Saŕr aliipatia bao la utangulizi Simba akipokea pasi nzuri ya kichwa kutoka kwa Kibu Denis baada ya krosi ndefu ya Luis Miquissone kutua kwenye kichwa chake na kutengeneza pasi ya usaidizi kwa Sarr. Geita Gold 0-1 Simba.

Geita Gold walilazimika kuifungua mechi ili wapate bao la kusawazisha walahu.

Walitengeneza nyakati mbili za mshtuko kwa Simba, Tariq Seif Kiakala aliunganisha kwa kichwa krosi nzuri ya Mwaita Gereza lakini mpira ukaenda nje kidogo ya lango, Manula akihakikisha.

Lakini dakika ya 90+2, Nassor Saadun alipokea pasi nzuri kutoka kwa Erick Mwijage lakini shuti lake likapaa juu kidogo ya lango.

Mpaka filimbi ya mwisho ya muamuzi wa mchezo Jonesia Rukyaa inapulizwa kutamatisha dakika zote 90, Geita Gold 0-1 Simba.

Makala Nyingine

More in NBC Premier League