Zanzibar imesifika sana kwa kuzalisha wachezaji wengi wenye vipaji ambao wamekuwa msaada mkubwa kwa klabu kadhaa zinazoshiriki Ligi kuu Tanzania Bara na timu ya Taifa ya Tanzania.
Moja ya nyota waliowahi kutamba nchini kutoka visiwani Zanzibar ni Amir Maftah, Nadir Haroub “Canavaro”, Feisal Salum, Ibrahim Hamad Abdallah, Maabad Maulid Maabad na wengine wengi.
Kwa miaka ya hivi karibuni nyota wengi wamesajiliwa kutokea visiwani Zanzibar, wengine wakiwa na mwendelezo mzuri na wengine kujikuta wanashindwa kuendana na kasi ya soka la Tanzania Bara licha ya ubora waliotoka nao Ligi ya Zanzibar.
Mohamed Ally ni mwandishi mkongwe wa michezo kutoka visiwani Zanzibar anasema moja ya changamoto wanayokutana nayo nyota kutoka visiwani ni kukaa kwa muda mrefu kambini wakisajiliwa na klabu za Tanzania Bara tofauti na Zanzibar ambapo hakuna kambi kwa klabu.
“Mfumo wa maisha wa klabu za Zanzibar na Tanzania Bara unatofautiana, asilimia kubwa ya klabu za Bara zinaishi mazingira ya kambi kwa muda mrefu maana yake ni kwamba asilimia kubwa ya maisha yao ni kambini”.
“Kwa upande wa Zanzibar, timu zinaingia kambini siku ya mchezo, unakuta wanakutana saa nne asubuhi hadi muda wa mechi, baada ya hapo kila mtu na maisha yake”.
“Aina hii ya mfumo ambao wachezaji wanatoka nayo huku, na kwenda kuanza aina nyingine ya maisha, na hasa ikiwa hujajiandaa kisaikolojia, linaweza kuwa ni kikwazo”, Alisema Mohamed Ally.
Maabad Maulid Maabad ni nyota ambaye amesajili wa na kikosi cha Coastal Union ya Tanga ambayo inashiriki Ligi kuu Tanzania Bara, wakati anasajiliwa alitoka kuwa mfungaji bora mara mbili wa Ligi kuu visiwani Zanzibar.
Baada ya kusajili na Coastal mwanzoni hakuwa kwenye kiwango kile alichokuwa nacho Zanzibar lakini kadri muda unavyosonga anazidi kuimarika zaidi, hapa anaeleza changamoto alizokutana nazo baada ya kutua Tanzania Bara.
“Changamoto kutoka ligi ya Zanzibar na Tanzania, kwanza lazima ufanye kazi kubwa mpaka kuaminika katika timu.”
“Huku watu wanakaa kambi tofauti na Zanzibar kila mtu na tabia yake”.
“Faida ya kukaa kambi mnapatikana kwa urahisi zaidi mkihitajika tofauti na kutokea nyumbani ya kukaa kambi”, Alisema Maabad Maulid Maabad.
Maabad anasema wachezaji kutoka Visiwani Zanzibar wanapaswa kupewa muda na kuamiwa zaidi ili wazoee mazingira na mwisho wa siku wafanye vizuri.
“Tunapaswa kupewa muda na kuaminiwa zaidi, lakini kukaa kambi hakuathiri kiwango cha mchezaji”, Alimalizia Maabad.