Taarifa kutoka nchini Rwanda zilikuwa zinaeleza kuwa mshambuliaji wa klabu ya Rayon Sport ya Rwanda Heritier Luvumba amevunjiwa mkataba na klabu hiyo baada ya kushangilia kwa mtindo wa kuziba mdomo na mkono mmoja kuuweka kichwani baada ya kuifungia timu yake goli kwenye mchezo wa Ligi kuu nchini Rwanda.
Ishara aliyoionyesha Luvumba inatumiwa na wachezaji wengi raia wa Congo DR wakipeleka ujumbe nchini kwao wa kusitisha mapigano na mauaji yanaoendelea mashariki mwa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa kadhaa zinasema kuwa nchi ya DR Congo na Rwanda hazichangamani kisiasa kutokana na shutma kadha wa kadha ambazo zinaelekezwa kwa pande zote kuhusu vita zinazoendelea nchini Congo DR.
Baada ya taarifa hiyo kuzagaa klabu ya Rayon Sport imetoa taarifa ambao imeeleza kuwa hawajavunja mkataba na nyota huyo na badala yake wamemkanya mchezaji huyo.
“Hatujavunja mkataba ma Luvumba, wengi hawajaelewa taarifa yetu tuliyoitoa baada ya tukio lile la ushangiliaji”.
“Sisi tumemkanya Luvumba na hatujavunja nae mkataba”.
“Rayon ni klabu ambayo haijihusishi na upande wowote ule wa kisiasa hivyo ni vyema wachezaji wetu waheshimu hilo”, Taarifa kutoka kitengo cha habari cha klabu hiyo.
Baada ya siku kadhaa kupita tangu taarifa ya kuvunjiwa mkataba itoke nyota huyo ameonekana kwenye viunga vya klabu ya AS Vita ya nchini kwao Congo DR akiwa anafanya mazungumzo na Rais wa klabu hiyo Amad Diallo.
Rais wa klabu hiyo amesema wapo tayari kumsainisha Luvumba ili aitumikie klabu hiyo na kama yupo tayari kusaini mkataba wake upo anaweza kusaini wakati wowote.
“AS Vita tupo tayari kumpa mkataba kama atakuwa tayari, Luvumba ni mchezaji mzuri na alikuwa anacheza Ligi mbovu ambayo haikuwa inamthamini”.
“Mkataba wake upo na kama atasaini leo basi kesho mapema ataonekana mazoezini”, alisema Rais wa AS Vita Club, Amad Diallo.