Connect with us

NBC Premier League

YANGA YAITANDIKA KMC, YAJIKITA KILELENI

Yanga wamezidi kujikita kileleni kibabe baada ya kuwanyuka KMC mabao 3-0 kwenye mchezo wa ligi kuu Tanzania bara uliopigwa kwenye dimba la CCM Jamuhuri, Morogoro na kufikisha alama 43 baada ya michezo 16.

Mpango wa KMC kuanza kucheza kuanzia chini uliwagharimu dakika za mapema kabisa baada ya kujikuta wanawazawadia wapinzani wao bao la mapema kupitia piga nikupige ya walinzi wa KMC wakitaka kuokoa shambulizi hilo na mpira kumdondokea Mfungaji Mudathir Yahya aliyepiga shuti kumshinda Wilbol Maseke.

KMC walijaribu kurejea mchezoni wakiendelea na mpango wao wa kumiliki mpira lakini bahati mbaya hapakuwa na mipango thabiti ya kujenga mashambulizi ya maana.

Yanga hawakukaa kimya, walishambulia kwa kasi pindi walipopata nafasi wakitumia sana mapana ya kiwanja kupiga pasi za ndani, Clement Mzize alipata nafasi 2 za wazi akiwa yeye na mlinda lango lakini mara zote, Wilbol Maseke alikuwa Imara.

Pacome Zouzoua na Mudathiri Yahya pia walipata nafasi kadhaa za kuutanua uongozi kwa Yanga kipindi hicho cha kwanza lakini bado hawakuwa makini kutumia nafasi zao.

Kwenda mapumziko wakiwa nyuma kwa bao 1-0 pengine ilikuwa nafuu kwa kwa KMC kutokana na namna walivyokuwa wakicheza, wakiwaruhusu sana Yanga kusogea golini kwao kutokana na uchezaji wao wa chini sana.

Yanga waliingia kipindi cha pili na badiliko moja, akipumzishwa Clement Mzize na kuingia Joseph Guede. Huku KMC wakiamua kumpumzisha Golikipa Wilbol Maseke na nafasi yake kuchukuliwa na Denis Richard.

Dakika ya 54, Mudathir Yahya aliwafungia Yanga bao la 2 baada ya kupokea pasi nzuri kutoka kwa mlinzi Nickson Kibabage na yeye kupasia tu nyavuni akifikisha bao lake la 6 msimu huu na la 2 kwenye mchezo wa leo. Muendelezo mzuri kwake.

Wakiwa wanajiuliza wamefikwa na nini KMC, Pacome Zouzoua akashindilia msumari wa 3 hapo hapo dakika ya 59, akipokea pasi nzuri nyingine tena kutoka kwa Nickson Kibabage, pasi yake ya 4 ya usaidizi msimu huu na ya 2 kwenye mchezo huu. Yanga wakawa mbele kwa mabao 3-0.

Kipigo hiki kikamfanya Kocha Moalin kufanya mabadiliko ya haraka, kuwaingiza Daruwesh Saliboko, Tepsie Evance na Kenny Ally Mwambungu kuchukua nafasi za Shabani Chilunda, Issa Ndala na Ibrahim Mohamed.

Yanga wakendelea kusukuma mchezo bado wakitengeneza nafasi zingine za mabao, Joseph Guede alipata nafasi lakini shuti lake liliokolewa vizuri na Denis Richard.

Stephane Aziz, Nickson Kibabage na Maxi Nzengeli walikwenda nje kuwapisha Augustine Okrah, Lomalisa Mutambala na Kennedy Musonda. Mabadiliko ya nafasi kwa nafasi.

Joseph Guede aliwekewa pasi ya usaidizi kwa kichwa kutoka kwa Kennedy Musonda na yeye kuunganisha kwa Kichwa lakini mpira ukaenda kugonga mtambaa panya.

Dakika ya 85, Joseph Guede tena alipenyezewa pasi sukari kutoka kwa Mudathir Yahya lakini akamnyima “Assist” baada ya shuti lake kuokolewa na Denis Richard akiwa anatazamana nae. Kona haikuzaa matunda.

Mpaka dakika zote 90 zinatamatika, Yanga waliibuka na ushindi wa mabao 3-0 mbele ya KMC ikiwa ni kwa mara ya 2 msimu huu wanawanyuka tena bila kuruhus bao lolote.

Makala Nyingine

More in NBC Premier League