Ihefu wamefanikiwa kuibuka na ushindi wa 2 mfululizo baada ya kuwafunga Geita Gold 2-1 kwenye mchezo wa ligi kuu Tanzania Bara uliochezwa kwenye uwanja wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Nyankumbu, Geita na kuwafanya kufikisha alama 19 wakisogea mpaka nafasi ya 10 huku Geita Gold wakisalia nafasi ya 13 na alama zao 16 baada ya kupoteza mechi 3 mfululizo.
Ihefu ikiwaa kwenye mabadiliko makubwa tangu mchezo wao wa ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Mtibwa Sugar walionekana kuimarika huku wakielewana zaidi ikiwa ni kikosi kilichosheheni nyota wengi wa kigeni.
Wakianza mchezo kwa kasi ile ile, Ihefu walitangulia kupata bao dakika ya 6 tu ya mchezo kupitia kwa mshambuliaji wake hatari Elvis Rupia akiunganisha kwa kichwa krosi murua kutoka kwa Marouf Tchakei akitokea upande wa kushoto.
Haikuwachukua muda sana Ihefu kuandika bao la 2 na safari hii Marouf Tchakei ndiye aliyekuwa kwenye eneo la umaliziaji akiunganisha krosi ya Hernest Malongo baada ya kugongeana vema na Elvis Rupia. Dakika ya 12, Ihefu wakawa mbele kwa mabao 2-0.
Joash Onyango alishindwa kuendelea na mchezo dakika ya 16 tu nafasi yake ikichukuliwa na Lenny Kissu.
Geita Gold walijaribu kuamka kuendana sawa na mchezo na kuwapunguza kasi Ihefu. Licha ya kutokuwa na ufanisi wa kutosha hasa eneo la kiungo kuanzisha mashambulizi. Wakaamua kuimarisha eneo hilo kwa kumuingiza Jonathan Ulaya nafasi ya Seleman.
Ihefu hawakutengeneza shambulizi lingine lolote la kumsumbua Sebusebu Samson tangu wafunge mabao yao mawili hali iliyowafanya Geita Gold kupata utulivu na kwenda mapumziko wakiwa nyuma kwa mabao 2-0 pekee.
Geita Gold walirudi kipindi cha pili wakiwa na kasi zaidi kama walivyomaliza kipindi cha kwanza, wakisukuma zaidi mashambulizi awamu hii huku tangu kutambulishwa kwa Jonathan Ulaya kwenye eneo la kiungo, palionekana kutulia zaidi eneo hilo. Wakati huo, Edmund John akichukua nafasi ya Saadun Nassoro amabaye hakuwa na kipindi cha kwanza kizuri.
Dakika ya 49, dakika 4 tu tangu kuanza kipindi cha pili, Geita Gold walirejesha bao 1 kupitia kwa Tariq Seif Kiakala akifunga bao lake la 2 mfululizo baada ya kupokea mpira wa krosi uliochongwa na Mwaita Gereza uliomshinda golikipa Khomeiny Zubery na yeye kuusukumia tu kimiani.
Ihefu nao walifanya mabadiliko dakika ya 64 wakiwapumzisha Amadu Momade na Emmanuel Boltha na nafasi zao kuchukulia na Morice Chukwu na Joseph Mahundi.
Mchezo ukionekana umeshika kasi kwa Ihefu kujitahidi kulinda uongozi wao huku Geita Gold wakipambana kujipapatua kusawazisha au kuondoka na Ushindi.
Licha ya mabadiliko kadhaa kufanyika lakini bado hayakuweza kubadili ubao wa matokeo na mchezo kumalizika kwa Ihefu kuibuka na ushindi wa mabao 2-1