Connect with us

NBC Premier League

JKT TANZANIA NA KMC HAKUNA MBABE, MTIBWA AKISOTA MANUNGU

JKT Tanzania walitangulia kupata goli kupitia kwa Najimu Magulu dakika ya 8 ya mchezo akipokea pasi kutoka kwa Sixtus Sabilo aliyefanya kazi nzuri ya kumpita mlinzi wa KMC.

Wazee wa Kipigo cha Kizalendo wangeweza kupata bao la pili kupitia kwa Danny Lyanga aliyeanza hii leo, lakini alishindwa kutumia vizuri nafasi aliyotengenezewa na Isamil Aziz kader.

Dakika ya 40, KMC walisawazisha kupitia kwa mshambuliaji wake mpya Shaaban Iddy Chilunda aliyetumia vizuri krosi ya chini chini iliyopigwa na Raheem Shomary.

JKT Tanzania Walipata nafasi ya kujiandikia bao la pili kupitia mkwaju wa penati dakika ya 44 baada ya Ismail Azizi Kader kuangushwa na Mlinzi Abdallah Saidi Lanso eneo la 18 na muamuzi kuamuru adhabu ya mkwaju wa penati ambao hata Hivyo golikipa Wilbol Maseke alifanya wokovu kabla ya Daruwesh Saliboko kusaidia kuuondosha mbali kabisa.

Timu zote zilienda mapumziko kwa sare ya bao 1-1

Kipindi cha pili KMC walianza kwa kasi wakishambulia mfululizo tangu aingia George Makang’aa ambaye alipata nafasi na kuachia shuti kali lakini likawa sambamba na golikipa Ayoub Suleiman.

Dakika ya 55 JKT Tanzania walifanya mabadiliko ya Kiufundi wakiongeza kazi eneo la kushambulia kwa kuwaingiza Shiza Kichuya na Edward Songo nafasi za Danny Lyanga na Ismail Aziz Kader.

Saidi Hamisi Ndemla alipiga shuti kali kupitia adhabu ya faulo lakini golikipa Wilbol Maseke alifanya kazi ya ziada kupkoa shuti hilo sambamba na mpira wa marejeo uliomkuta Sixtus Sabilo. Walipoteza nafasi ya wazi JKT Tanzania dakika ya 76.

JKT Tanzania watajutia wenyewe kushindwa kupata matokeo ya ushindi kwenye mchezo huu baada ya kupoteza nafasi nyingi za wazi. Matheo Anthony alitengewa pasi nzuri sana na Saidi Ndemla, akiwa peke yake akajikuta anampa kipa dakika ya 89 ya mchezo.

Mchezo ukimalizika kwa sare ya 1-1 na kufanya KMC kuendelea kusalia kwenye nafasi yao ya 5 wakifikisha alama 24 huku JKT wakisogea hadi nafasi ya 12 wakifikisha alama 18 sawa na Tabora United.

Kwingineko, Kwenye dimba la Manungu Complex huko mkoani Morogoro, Mtibwa Sugar walitoka suluhu ya 0-0 na Dodoma Jiji.

Timu zote mbili licha kuonekana kucheza vizuri na kutengeneza nafasi kadhaa lakini walinda mlango wote wawili walikuwa na nyakati nzuri.

Baada ya Mchezo Kocha Francis Baraza alisema

Mimi nawapongeza Vijana wangu na nashukuru kwa alama hii 1. Tulikuja na mpango wetu mzuri wa kutaka kucheza eneo la kiungo lakini wenzetu nao walikuja na mpango wao tofauti hivyo ikatufanya na sisi tubadilike. Tutaenda kufanyia kazi hayo machache ya Leo ili tujue namna ya kutatua vitendawili kama hivi.

Naye Kocha wa Mtibwa Sugar Zubery Katwila alisema

Mechi ilikuwa nzuri, vijana wamecheza vizuri na wametengeneza nafasi lakini hatukuweza kutumia. Tunafanya kazi kubwa sana mazoezini na hata kiwanjani lakini ni lazima tukicheza kama hivi tufunge magoli ili tupate alama 3. Hatupo kwenye nafasi nzuri lakini inabidi tusikate tamaa tuweke saikolojia yetu sawa, tuendelee kupambana.

Mtibwa Sugar wanafikisha alama 9 wakiendelea kuburuta mkia kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara huku Dodoma Jiji wakisalia nafasi yao ya 10 wakifikisha alama 20.

Makala Nyingine

More in NBC Premier League