Afisa habari na mawasiliano wa klabu ya Simba Ahmed Ally ameendelea na hamasa kwa mashabiki wa klabu hiyo kuelekea mchezo wao wa Ligi ya mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy.
Mchezo huo utapigwa jumamosi hii katika uwanja wa Benjamini Mkapa, Jijini Dar Es Salaam huku akiwahakikishia mashabiki wa klabu hiyo kuwa watautumia mchezo huo kufuzu hatua ya robo fainali kama ilivyo kwa majirani zao klabu ya Yanga.
“Jumamosi tunakwenda kuingia robo fainali kwa mara ya tano mfululizo, kwetu sisi kuingia robo ni jambo la kawaida. Tumezoea kucheza robo na hatujawahi kuishia makundi tangu tumeanza kampeni yetu ya kimataifa.”
“Tulimuua AS Vita wa moto, tulimuua USGN, tulimuua Horoya hatuwezi kushindwa kwa Jwaneng Galaxy. Simba anapoitaka robo fainali hakuna wa kutuzuia hata timu zingine zote duniani zitengeneze timu moja. Jwaneng amekuja wakati mbaya, muda ambao tunataka kulipiza kisasi.”
“Lilitukaa rohoni lakini muda wa kumtemea nyongo Jwaneng Galaxy, tulikaa na maumivu kwa miaka mitatu na la pili tunataka kuingia robo fainali. Hatuwezi kufungwa na timu inayoburuza mkia katika kundi letu.”
“Tutafanya kila kinachowezekana ilimradi Simba ipate ushindi siku hiyo na hakuna kinachoshindikana. Iwe ardhini, angani au chini ya bahari.”
“Tunawaahidi na kuwahakikishia Wanasimba kama kuna kitu kinahitajika hata kiwe kinapatikana chini ya bahari tutakifanya ili Simba iende robo fainali. Jumamosi ni kwenda kumalizia kazi.” Ahmed Ally.
Mchezo wa Simba na Jwaneng Galaxy utapigwa saa moja kamili [19:00] kwa saa za Afrika Mashariki na ni mchezo muhimu zaidi kwa Simba kushinda.