Ihefu wameshindwa kutamba kwenye Uwanja wao mpya waliohamia wa CCM Liti uliopo mkoani Singida baada ya kulazimishwa Sare na bao 1-1 na Mashujaa kwenye mchezo wa ligi kuu Tanzania Bara.
Elvis Rupia aliitanguliza Ihefu dakika ya 11 ya mchezo akiunganisha kwa kichwa krosi maridadi ya Mangolo.
Dakika ya 19 Duke Abuya alimsetia Elvis Rupia pasi nyingine akiwa karibu na golikipa na Erick Johora lakini tayari alikuwa amekwisha otea.
Ihefu walionekana kuwa kwenye usukani wa mchezo wakiwashambulia sana Mashujaa ambao hawakuwa wakitengeneza nafasi nyingi. Adam Adam hakupata nafasi nyingi za wazi za kufunga.
Marouf Tchakei, Duke Abuya na Lobotha. walionekana kucheza kwa kuelewana zaidi kwenye eneo la kiungo pengine kutokana na kucheza pamoja kwa muda mrefu walikotoka, wakimpa usaidizi mkubwa Elvis Rupia licha ya Said Makapu na Mgandila kujaribu kuzuia mashambulizi.
Mapumziko Ihefu walikuwa mbele kwa bao 1-0.
Kipindi cha pili kilionekana kina uwiano sawa baada ya Mashujaa kurejea kwa kasi.
Dakika ya 73, Omary Omary aliisawazishia Mashujaa akiunganisha kwa kichwa pasi nzuri ya usaidizi kutoka kwa Adam Adam na kumfanya Aboubakar Komeihny asiwe na la kufanya.
Ihefu waliamua kufanya mabadiliko kwa kuwaingiza Ezekiel Mwashilindi na Joseph Mahundi kuongezea nguvu eneo lao la kiungo ambalo lilionekana kuzidiwa, nje alikwenda Morice Chukwu. Lakini Jafary Kibaya na Ismail Mgunda waliingia Kuboresha eneo la ushambuliaji.
Licha ya mabadiliko yote kufanyika, bado Ihefu hawakuweza kupata bao la ushindi kwenye mchezo huu wa kwanza nyumbani kwenye uwanja wao mpya. Dakika zote 90 zikatamatika kwa Sare ya bao 1-1.
Matokeo haya yanawafanya wote wawili kubaki kwenye nafasi zao, Ihefu wakisalia nafasi ya 11 wakiwa na alama zao 20 huku Mashujaa wakisalia nafasi ya 15 wakiwa na alama zao 15. Alama 1 nyuma ya Geita Gold.
Kwingineko kwenye dimba la Sokoine, Mbeya, wenyeji Tanzania Prisons walifanikiwa kuvuna alama zote 3 baada ya kuwafunga Tabora United kutoka mkoani Tabora kwa mabao 2-1.
Tabora United walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa Erick Okutu dakika ya 17 lakini dakika 4 tu baadae, Dakika ya 21, Zabona Mayombya aliisawazishia Prisons huku akifunga bao lake la 3 ndani ya mechi 3.
Dakika ya 88, Samson Mbangula aliwainua wajelajela kwa kuandika bao la 2 na la ushindi kwa timu yake na kuhakikisha alama zote 3 zinabaki Mbeya.
Kwa matokeo haya, Prisons wanawashusha KMC nafasi ya 5 na kukaa wao wakifikisha alama 24 sawa nao lakini wakiwazidia kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa huku Tabora United wakipanda hadi nafasi ya 12 kutoka nafasi ya 13, JKT Tanzania wakiwa na mchezo mmoja pungufu.