Connect with us

CAF Champions League

SIMBA YAIFUMUA JWANENG GALAXY, YATINGA ROBO FAINALI

Simba wamefanikiwa kuingia hatua ya Robo Fainali ya michuano Ligi ya Mabingwa baada ya kuifumua Jwaneng Galaxy kwa mabao 6-0 kwenye mchezo uliopigwa kwenye dimba la Benjamin Mkapa.

Simba walianza mchezo kwa kasi na dakika ya 7 tu Saido Ntibazonkiza aliitanguliza timu yake akimalizia vizuri kazi nzuri kabisa ya Clatous Chama aliyepiga pasi ya ndani akitokea upande wa kushoto.

Jwaneng Galaxy ni kama walianza kutoka mchezoni baada ya kuruhusu bao hilo huku likiwa limewatoa kwenye mpango wao.

Simba walitumia mwanya huo kupachika bao la 2 dakika ya 14 baada ya nipe nikupe nzuri ya Clatous Chama na Saido Ntibazonkiza kabla hajatoa pasi mserereko kwa Pa Omar Jobe ambaye hakufanya ajizi mbele ya golikipa Phoko.

Wakiwa bado wanajiuliza wamepigwa nini huku wakizidi kutoka kwenye mpango wao, Dakika ya 22 alikuwa ni Kibu Denis aliyeitendea haki Pasi ya Clatous Chama ambaye alishawatambuka walinzi wa Jwaneng Galaxy kupiga shuti lililonasa kambani na kutanua wigo wa uongozi kwa Simba hadi 3-0.

Ingeweza kuwa 4-0, 5-0 lakini haikuwa hivyo. Clatous Chama alipata nafasi 2 za wazi akiwa anatizamana na golikipa lakini mashuti yake yote yalilenga nguzo ya chini ya kushoto hata goli alilofunga kutokana na mpira rejeo kutoka kwa Kibu Denis alikuwa amekwisha otea.

Jwaneng Galaxy walimaliza kipindi cha kwanza bila kuwa na shuti lolote lililolenga lango. Huku Simba wakionekana kuitawala “scoreboard” kwa kwenda mapumziko wakiwa kifua mbele kwa mabao 3-0.

Jwaneng Galaxy walirudi kipindi cha pili wakiwa na utulivu kujaribu kupooza kasi ya mashambulizi ya Simba lakini ni kama vile Simba hawakuwa na mpango wa kupoa wakati wowote ule.

Clatous Chama alipata bao lake dakika ya 76 ya mchezo akipokea pasi murua kabisa kutoka kwa Saido Ntibazonkiza na kumpigia golikipa mbali kabisa ambapo hakuweza kufika.

Simba walifanya mabadiliko wakiingia Ladack Chasambi, Luis Miquissone na Freddy Kouablan wakichukua nafasi za Kibu Denis, Saido Ntibazonkiza na Pa Omar Jobe.

Dakika ya 86, ikiwa dakika 6 tu tangu aingie, Ladack Chasambi aliifungia Simba bao la 5 akipokea pasi nzuri ya Freddy Kouablan akiwa kafanya kazi nzuri na yeye kukandamiza msumari wa 5. Simba walikuwa kwenye siti ya mbele.

Simba walionekana kutotosheka kabisa na magoli na kuendelea kulisakama vilivyo lango la Jwaneng Galaxy.

Dakika ya 90, Simba walipata bao la 6 kupitia kwa Fabrice Ngoma aliyeunganisha vizuri kwa kichwa krosi ya Mohamed Hussein.

Ingewezekana Simba kupata mabao zaidi kwani Jwaneng Galaxy walikuwa tayari dhohofu. Simba walionekana kuutawala mchezo wote mpaka dakika ya mwisho ya mchezo.

Mchezo ulimalizika kwa Simba kupata ushindi mnono wa mabao 6-0.

Makala Nyingine

More in CAF Champions League