Azam FC na Coastal Union wamegawana alama 1 kila upande baada ya kutoka sare 1-1 kwenye mchezo wa ligi kuu Tanzania Bara mchezo uliopigwa kwenye dimba la Azam Complex, Chamazi. Matokeo ambayo yamewafanya Azam Kuongoza ligi wakiwa na alama 44 baada ya mechi zao 20 huku Coastal Union wakirejea nafasi yao ya 4 wakifikisha alama 27.
Mchezo ulikuwa mgumu kwa timu zote kuanza mchezo kwa kusikiliziana huku wakishambuliana kwa kushitukiza.
Hapakuwa na matukio mengi ya kuripoti kipindi cha kwanza, walinda milango wote wawili walikuwa makini sana kusoma nyakati na matukio.
Ibrahim Ajibu alipata kupiga faulo nje kidogo ya eneo la Azam FC lakini pigo lake likapaa juu kidogo ya lango.
Mapumziko timu zote zilienda kwa suluhu ya 0-0.
Azam walirejea kipindi cha pili na mabadiliko, wakitambulishwa mchezoni James Akaminko na Gybrill Sillah nafasi za Adolf Mtesigwa na Iddy Nado.
Dakika ya 47, Yannick Bangala alifunga bao kwa kichwa akiunganisha krosi nzuri ya Ayoub Lyanga lakini tayari alikuwa kwenye eneo la kuotea.
Coastal Union waliendelea kucheza kiutulivu sana huku wakiwaheshimu Azam ambao walikuwa wamefanya mashambulizi mengi mfululizo bila kuzaa matunda.
Dakika ya 68, Daud Charles Semfuko aliwatanguliza Coastal Union kufuatia mpira wa kona aliounganisha vizuri kwa kichwa na kufanya ubao usomeke 1-0 faida kwa Coastal Union.
Azam walicharuka na kuwashambulia vilivyo Coastal Union. Dakika ya 70, Pascal Msindo alimlazimisha Ley Matambi kufanya uokovu mara mbili kumkatalia bao.
Daikka ya 71, Ley Matampi tena alimkatalia Feisal Salum shuti lake tena kuiweka Coastal Union salama nyakati hizi.
Mashambulizi hayakupoa, Matampi tena alifanya uokovu mara mbili kukata shuti la Yannick Bangala ndano ya 6 kabla ya kuokoa tena kichwa cha Gybrill Sillah. Matampia alifanya uokovu mara 5 ndani ya dakika 6.
Hatimae dakika ya 80, Feisal Salum aliandika bao lake la 12 msimu huu na bao la kusawazisha kwa Azam akipokea pasi nzuri kutoka kwa Kipre Jr. akitokea upande wa kulia na yeye kuusokomeza tu kimiani, mara hii Matampi akiwa hana la kufanya.
Coastal Union walifanya mabadiliko wakimtambulisha Chrispin Ngushi nafasi ya Modzaka huku Ibrahim Ajibu akimpisha Lucas Kikoti.
Almanusura Fuentes Mendoza aiandikie timu yake ya Azam bao la ushindi dakika ya 90, kupitia mpira wa kona lakini shuti lake likagonga mtambaa panya, Coastal Union wakaendelea kubaki salama.
Dakika zote 90 zikatamatika kwa Azam kutoka sare ya 1-1 dhidi ya Coastal Union.