Tanzania Prisons wamefanikiwa kuibuka na alama zote 3 baada ya kuwaduwaza Simba kwa kuwanyuka mabao 2-1 kwenye mchezo wa ligi kuu Tanzania Bara uliopigwa uwanja wa Jamhuri, Morogoro matokeo yaliyowafanya Prisons kusogea hadi nafasi ya 4 baada ya kufikisha alama 27 kwenye michezo 19 waliocheza.
Simba walidhani wamepata bao la utangulizi kupitia kwa Fabrice Ngoma aliyepokea mpira uliokuwa umebabatiza shuti kutoka kwa Kibu Denis lakini alikuwa kwenye nafasi ya kuotea tayari.
Tanzania Prisons walitangulia kupata bao kupitia kwa Samson Mbangula baada ya kupokea pasi ndefu kutoka kwa Joshua Nyantini wakati Simba wanafanya shambulizi, akajitangulizia pasi ndefu kisha kupiga shuti kali lililomshinda golikipa Aishi Manula.
Simba licha ya kuonekana kumiliki sana mchezo lakini hawakuwa wakatili kwenye kuzitumia nafasi zao hali iliyozidi kuwapa kujiamini walinzi wa Prisons ambao hata hivyo walicheza vizuri.
Kipindi cha Kwanza Kilimalizika kwa Prisons kuwa mbele kwa bao 1-0.
Simba walirejea kipindi cha pili kwa kufanya mabadiliko, Ladack Chasambi, Pa Omar Jobe na Saido Ntibazonkiza waliingia kuchukua nafasi za Kibu Denis, Freddy Kouablan na Mzamiru Yassin.
Prisons waliendelea kuwa imara kwenye lango lao, wakidhibiti Mashambulizi ya Simba lakini pia wakitumia mashambulizi ya kujibu wanapopata mwanya wa kutoka golini kwao.
Alikuwa ni Samson Mbangula tena aliwatepetesha walinzi wa Simba kabla ya kupiga shuti lililopita katikati ya miguu ya Aishi Manula na kuiandikia timu yake bao la 2 na la kwake la 2 kwenye mchezo huu akifikisha mabao 6 ndani ya mechi 6. Simba 0-2 Prisons.
Prisons walimpumzisha Samson Mbangula na kumuingiza Chillo Mkama ili kwenda kuimarisha safu ya Ulinzi kuendelea kulinda uongozi wao.
Clatous Chama alipiga pigo la adhabu lililoenda kugonga nguzo lakini Israel Mwenda alishindwa kumalizia mpira rejeo na kuikosesha timu yake kupata bao la kusawazisha.
Lango la Prisons liliendelea kubaki salama mpaka dakika ya 89 ya mchezo waliporuhusu bao lililofungwa na Fabrice Ngoma akitumia mpira wa kona uliopigwa na Edwin Balua aliyeingia nafasi ya Babacar Saŕr.
Hata Hivyo Prisons walifanikiwa kuulinda Uongozi wao mpaka dakika ya mwisho ya mchezo na kufanikiwa kuondoka na ushindi wa mabao 2-1
KWINGINEKO kwenye dimba la Lake Tanganyika, Kigoma, Mashujaa wamefanikiwa kutwaa alama zengine 3 mbele ya ndugu zao JKT Tanzania baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0.
Bao pekee la mchezo huo lilipatikana dakika ya 7 ya mchezo kupitia kwa Balama Mapinduzi na kudumu kwa dakika zote 90.
Matokeo haya yanainasua Mashujaa kutoka nafasi ya 15 mpaka nafasi ya 11 wakifikisha alama 21 huku wakiishusha JKT Tanzania.