Tanzania imebarikiwa kuwa na watu wengi ambao wanafanya kazi ya kufundisha [Kocha] timu mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na timu za Ligi kuu, Championship, Ligi daraja la kwanza na madaraja mengine.
Kwenye wingi wa makocha hao wapo ambao wamefanya vyema kwenye nafasi zao na wanatambulika kutokana na kazi njema walizozifanya.
Mchambuzi na mtangazaji wa mpira nchini Gharibu Mzinga amemtaja kocha Meja mstaafu Abdul Mingange kuwa ndiye kocha wake bora wa muda wote mzawa aliyewahi kufundisha nchini.
“Kwangu mimi ni Meja mstaafu Abdul Mingange ndiye kocha bora mzawa kuwahi kufundisha Ligi kuu Tanzania Bara,” – Gharibu Mzinga
Kocha Abdul Mingange amewahi kufundisha nchini klabu zinazoshiriki Ligi kuu na Championship kwa wakati tofauti ambazo ni pamoja na Azam FC, Mbeya City, Mashujaa na klabu nyingine nyingi.
Kocha Meja mstaafu Mingange ameweka wazi kuwa ubora wake umetokana na kozi nyingi ambazo walikuwa wanazipata wakati wa kipindi chao.
“Sisi tulikuwa tunapata kozi nyingi sana kutoka FIFA, kutoka UEFA na kutoka CAF, kila baada ya miezi miwili au mitatu mnapata kozi, zile zilitujenga sana.”
“Vijana wetu hawa hawapati kozi nyingi zaidi ya kusoma leseni na kufanya “refresher” hawapati muda mwingi wa kupata mawazo tofauti tofauti.”
“Toka nimeanza kujifunza tangu mwaka 1987 hadi leo we unategemea nina ufahamu [Knowledge] kiasi gani ?.” – Meja Mstaafu Abdul Mingange.
Kwasasa kocha huyo hana timu anayoifundisha tangu alipoachana na klabu yake ya zamani ya Mashujaa ambayo aliachana nayo mara baada tu ya kuipandisha daraja na yupo tayari kufundisha klabu yoyote itakayomuhitaji.
“Mimi huwa sipendi kuomba lakini timu ikija mimi naenda, timu yoyote wakati wowote itakaponihitaji mimi nipo tayari kuungana nao.” – Kocha Meja Mstaafu Abdul Mingange.