Kocha wa Klabu ya Yanga Miguel Gamondi amesema kuwa timu yake iko tayari kwa mapambano dhidi ya Mamelodi Sundowns watakapokutana kwenye mchezo wa marudiano hapo kesho.
Tunajua zitakuwa dakika 90 ngumu sana lakini uzuri bado ni mchezo ambao upo 50/50 na yoyote anaweza kushinda mchezo huu na hivyo tuko hapa kuhakikisha tunapambana na kushinda mchezo huu. Kwa namna ambavyo tumejiandaa mazoezini haitokuwa mechi nyepesi kwetu wala kwao pia.
Kocha Gamondi alielezea pia kuhusu ari na uzoefu wa wachezaji wake kuelekea mchezo huo.
Tuna wachezaji wazoefu kama mtakumbuka msimu uliopita walipambana sana kwenye Kombe la Shirikisho, licha ya kupoteza Nyumbani lakini wote mnakumbuka nini kilitokea ugenini. Japo huu ni mchezo tofauti lakini nawaamini na nimeiona ari yao ya kutaka kushinda na kupambana tena kwa ajili ya mashabiki.
Aidha hakuacha kuzungumzia uzoefu wake binafsi:
Sio mara yangu ya kwanza kuja hapa, nishawahi hata kuwa kocha hapa. Mara ya mwisho nilikuja na Platinum na tukashinda 2-1 dhidi yao. Ninaheshimika nchi hii lakini safari hii nimekuja na Young Africans na lengo ni kuwafurahisha Watanzania.
Kwa umuhimu pia aligusia hali ya majeruhi:
Najua tuna mchezo muhimu wa kufuzu nusu fainali lakini pia hii sio mechi ya mwisho(ya msimu) nina mashindano mengine hivyo siwezi kuhatarisha afya za wachezaji wangu kisa mchezo mmoja hivyo tutaangalia mazoezini kama tutapata mchezaji ambaye atakuwa tayari kwa mchezo kati ya majeruhi waliopo. Lakini sitoharakisha.
Young Africans watawavaa Mamelodi Sundowns kwenye dimba la Loftus, Pretoria juma moja tangu watoke suluhu ya 0-0 jijini Dar es Salaam kwenye dimba la Mkapa.
Mshindi wa jumla atafuzu kwenda hatua ya Nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.