Connect with us

Makala Nyingine

KONGOLE SIMBA NA YANGA, JUHUDI ZIMEONEKANA.

Timu za Simba na Yanga kutoka Tanzania zimeondolewa kwenye Mashindano ya Ligi ya Mabingwa wa Vilabu Afrika baada ya kupoteza michezo yake kwenye hatua ya Robo Fainali ya Michuano Hiyo.

Young Africans walitolewa kwa njia ya Mikwaju ya Penati na Mamelodi Sundowns 3-2 baada ya michezo yote miwili kumalizika kwa suluhu ya 0-0.

Simba upande wao walitolewa na Al Ahly kwa jumla ya mabao 3-0, wakiruhusu kufungwa nyumbani 1-0 na kufungwa mabao 2-0 ugenini kwenye dimba la Cairo International.

Licha ya timu zetu zote mbili kutolewa lakini zimeonyesha ukomavu na upambanaji wa hali ya juu na kudhihirisha kuwa soka la Tanzania hakika linakuwa kwa kasi.

Rekodi ya kwa mara ya kwanza kupeleka timu 2 hatua ya Robo Fainali ya mashindano haya na ikiwa ndio nchi pekee kutoa wawakilishi wawili msimu huu, haitosahaulika kwenye akili za watanzania.

Young Africans wakishiriki kwa mara ya kwanza hatua ya Robo Fainali walionyesha kuwa na timu bora sana msimu huu wakicheza kwa mikakati mikubwa dhidi ya timu inayozungumzwa sana kiubora, Mamelodi Sundowns na kuhenyeshana nao mpaka hatua ya Penati.

Simba nao hawakuonyesha unyonge mbele ya Al Ahly kwani licha ya kutolewa lakini walionyesha ukomavu wao kwenye mashindano haya wakiwamiliki vilivyo wapinzani wao ila wakionekana kukosa ubora hasa kwenye eneo lao la umaliziaji.

Kuna mstari mwembamba sana unaozitenganisha timu zetu na hatua ya Nusu Fainali. Ni kwenye eneo la kuzidisha ubora wa Sajili, kuleta wachezaji wa madaraja makubwa wenye uwezo wa kuamua michezo migumu kama hii. Simaanishi kwamba hatuna baadhi yao ila tunahitaji kuongeza wengine zaidi ili kupunguza mwanya uliopo kati ya wachezaji wanaoanza na wanaoingia.

Heshima Kubwa pia kwa mashabiki wachache ambao walijitokeza kutoa hamasa kwa wachezaji wa timu zetu zote hizi. Hakika mmeupiga mwingi sana.

Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Dr. Samia Suluhu Hassan ametoa Kongole kwa Timu zote hizi mbili huku akiendelea kuahidi kuzipa motisha akiamini kuna hatua chache sana kufikia kilele cha mafanikio.

Na sisi hapa kama Daudasports Tunatoa heshima hizo hizo kwa timu zetu kwa kupambania Taifa vilivyo. Wakati ujao ni wakati bora zaidi.

Makala Nyingine

More in Makala Nyingine