Connect with us

NBC Premier League

MZANI SAWA GEITA GOLD NA MTIBWA SUGAR

Goli la dakika za jioni la Omary Marungu lilitosha kuipa alama 1 muhimu ugenini Mtibwa Sugar kwenye mbio za kupambania kusalia ligi kuu baada ya kutoka sare ya 2-2 dhidi ya Geita Gold kwenye dimba la Nyankumbu.

Mtibwa Sugar walionyesha kuutaka mchezo mapema kabisa wakicheza kwa kasi na kutengeneza mashambulizi kadhaa dakika za mwanzo za mchezo.

Juhudi ziliwalipa Mtibwa dakika ya 15 walipoandika bao kupitia kwa Jimmyson Mwanuke aliyepokea mpira ambao haukuokolewa vizuri na walinzi wa Geita Gold na kuachia shuti kali lililomshinda Yusuph Ally.

Geita Gold wakaamka na kuonyesha dhamira ya kutaka kusawazisha bao hilo wakifanya kila aina ya jitihada na kuifanya Mtibwa Sugar kushuka chini.

Shinikizo likalipa baada ya Geoffrey Julius kufanyiwa madhambi kwenye eneo la 18 akiwa analielekea lango la Mtibwa Sugar na Mwamuzi Nassor Mwinchui kuamuru mkwaju wa penati uliowekwa kimiani kiustadi kabisa na Yusuph Mhilu kuufanya mzani kuwa sawa 1-1 dakika ya 21.

Mtibwa Sugar waliendelea kuwekwa hatiani, Yusuph Mhilu, Offen Chikola na Valentino Mashaka wakiwasiliana vizuri sana Geoffrey Julius kutengeneza hatari nyingi.

Dakika ya 36, Valentino Mashaka alitumia uzembe wa golikipa Ndikumana aliyeshindwa kuudaka mpira wa Faulo uliochongwa na Mlingo na yeye kuukwamisha mpira wavuni kuwapa Geita Gold uongozi waliostahili. 2-1 mpaka mapumziko.

Kipindi cha pili Mtibwa Sugar walirejea tofauti safari hii wakiwa wao timu kinara kiwanjani kama walivyoanza kipindi cha kwanza lakini wakicheza pasi fupi fupi eneo la kiungo likiongozwa vema na Nassor Kapama na Jimmyson Mwanuke.

Mtibwa Sugar walifanya mabadiliko na kuwaingiza Seif Karihe na Omary Marungu.

Haikumchukua muda Marungu kutambulisha uwepo wake kwani dakika 2 tu tangu aingie alitumia vema kabisa krosi murua iliyochongwa na Kazi na kuunganisha kwa kichwa kuweka mzani sawa. 2-2.

Mpaka dakika zote 90 zinatamatika, Timu zote mbili ziligawana alama 1.

Makala Nyingine

More in NBC Premier League