Young Africans wameendelea kujizatiti kileleni wakipata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Singida FG na kufikisha alama 55 kwenye mchezo uliopigwa kwenye dimba la CCM Kirumba, Mwanza.
Licha ya kuwa uwanja haukuwa na mazingira mazuri kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha, bado haikuzuia timu hizi mbili kutupa mchezo mzuri kila timu ikionyesha dhamira ya kuvuna alama 3.
Alikuwa ni Joseph Guede dakika ya 41 aliyefungua karamu ya mabao kwa Young Africans alipoitanguliza kwa bao maridadi akitumia vizuri pasi ya Joyce Lomalisa Mutambala na kuuzungusha mpira mwamba wa mbali kabisa na mpira kumshinda Benedict Haule.
Mapumziko Young Africans walikuwa mbele kwa bao 1.
Kipindi cha pili hakikuwa tofauti sana na cha kwanza, licha ya kuwa Nyuma bado Singida FG walionyesha ari ya kupambana kutaka kusawazisha bao.
Dakika ya 65, Stephane Aziz Ki alinyunyiza chumvi kwenye Kidonda cha Singida FG akitumia vema pasi ya Clement Mzize na kupiga shuti la mbali lililomshinda Haule kuiandikia Yanga bao la 2.
Wakati wakijiuliza wamepigwa na nini, Joseph Guede dakika ya 67 alitumia vema tena pasi ya usaidizi ya Clement Mzize kuiandikia Yanga bao la 3 na la kwake la 2 kwa Kichwa kulizamisha kabisa Jahazi la Singida FG.
Dakika zote 90 zikatamatika kwa Yanga kuibuka na alama zote 3 wakipata ushindi wa mabao 3-0.
Baada ya mchezo kumalizika, Kocha msaidizi wa Singida FG Ngawina Ngawina alikuwa na haya ya kusema
Unapocheza na Timu yenye wachezaji wenye ubora kama Yanga unalazimika kutofanya makosa mengi maana kila kosa watakuadhibu. Tulicheza vizuri dakika za mwanzo lakini mpaka dakika ya 40 tukafanya kosa tukafungwa. Kipindi cha pili pia dakika za 60 tulikuwa tuko vizuri ila makosa mawili ya haraka yakatuadhibu. Hili limeisha tunajipanga na mchezo ujao dhidi ya Ihefu tarehe 18.
Upande wa Yanga alizungumza Dickson Job
Hapa tulikuwa tunapigania alama 5 kwa haraka haraka na tunashukuru tumezipata. Haukuwa mchezo mrahisi na sio tu kwasababu ya wapinzani wetu bali hata uwanja haukuwa vizuri sana lakini tumepambana kupata alama hizo ambazo ni muhimu sana kuelekea kwenye ubingwa. Tunachukua mechi moja moja kufikia malengo yetu.