Moses Armah “Parker” ni mfanyabiashara, na Rais wa klabu ya Medeama ya nchini Ghana ambayo inashiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu huu ikiwa kundi moja pamoja na klabu ya Young Africans.
Parker aliinunua klabu ya Kessben kwa ada ya US $ 600,000 na baadae kuibadili jina na kuwa Medeama hii ambayo sote tunaifahamu.
Katika uchaguzi mkuu wa shirikisho la soka nchini Ghana mwaka 2019, Moses Armah aliiwakilisha klabu ya Medeama na kupiga kura kwa niaba ya klabu hiyo.
Mwaka 2014 kwenye fainali za kombe la Dunia nchini Brazil, vyombo kadhaa vya habari nchini Ghana vililipoti kuhusu ugomvi wake mkubwa na mchezaji wa zamani wa AC Milan Sulley Ali Muntari.
Baadae mwaka 2016 wakati akihojiwa na chombo kimoja cha habari nchini Ghana Armah alisema kuwa amemsamehe Muntari kwa tukio hilo.
Kama una kumbuka mwaka huo huo Muntari na Kevin Prince Boateng waliondolewa kwenye kambi ya timu ya Taifa kutokana na tukio hilo.
Kocha wa zamani wa Ghana James Kwesi Appiah aliweka wazi tukio hilo kwenye kitabu chake cha “Leader Don’t have to Yell”.
Baada ya kuichukua Medeama mwaka 2010, Moses Armah ameipandisha nembo ya klabu hiyo, wameiwakilisha Ghana mara mbili [2] kwenye kombe la shirikisho, mwaka 2014 na 2016, huku ikishiriki pia Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2023.
Alianzisha pia klabu ya Wassaman FC ambayo July 2013 ilibadilishwa jina na kuitwa Emmanuel Stars FC baada ya kununuliwa na mchungaji wa Nigeria TB Joshua.