Simba Queens wamefanikiwa kuwanyuka watani wao Yanga Princess kwa jumla ya mabao 3-1 na kufanikiwa kukusanya alama 3 muhimu na kujikita nafasi ya 2 nyuma ya JKT Queens wakiwa nyuma yao kwa tofauti ya magoli 5 wakiwa na alama sawa, 9.
Mchezo ulianza kwa kasi hasa kwa upande kwa upande wa Simba Queens ambao walionekana watulivu kwenye kujenga mashambulizi yao.
Dakika ya 2 tu ya mchezo, Simba Queens walipata bao la kuongoza kupitia kwa mshambuliaji wao hatari Aisha Mnunka. Fatuma Issa aligongeana vizuri na Viviane Corazon kabla ya kupiga pasi pembeni kwa Elizabeth Wambui ambaye naye alipagi pasi tamu kwa mfungaji. 1-0 Simba Queens.
Yanga Princess walipata mpira wa adhabu nje kidogo ya eneo ya Simba Queens lakini pigo la Precious Christopher halikulenga lango.
Dakika ya 10 Simba Queens walipata bao la 2 kupitia kwa Aisha Mnunka tena akipokea pasi nzuri kwa mara nyingine kutoka kwa Elizabeth Wambui ambaye mpira wake ulishindwa kuzuialiwa vizuri na Golikipa wa Yanga Safiatu Salifou na kumkuta mfungaji aliyeonekana kuwa mwimba mchungu kwa Yanga Princess leo.
Yanga Princess walipata bao la 1 la kuwarejesha mchezoni punde tu. Makosa ya Golikipa wa Simba Carolyene Rufaa kushindwa kwenda kuucheza mpira wa krosi wa Precious Christopher ulimpa nafasi Neema Paul kupiga mpira wa kichwa uliotinga nyavuni moja kwa moja. Simba 2-1 Yanga, dakika ya 15.
Licha ya mchezo kurejea kwenye ukawaida baada ya Yanga kupata goli 1 bado Simba Queens walionekana kuutawala zaidi mchezo huku Viviane akionekana kuwa bora zaidi eneo la kiungo pamoja na Danai Bhobho na Ritticia Nabbosa wakiwapoteza kabisa Irene Kisisa, Precious Christopher na Saiki Atinuke wa Yanga.
Asha Djafar alipokea pasi nzuri kutoka kwa Viviane Corazon lakini alishindwa kuitumia nafasi hiyo shuti lake likienda nje kidogo ya lango.
Yanga Princess walifanya mabadiliko ya mapema wakimtoa mfungaji wa bao Neema Paul na Anasatazia Shau.
Simba Queens waliendelea kuumiliki mchezo kwenye kila eneo la kiwanja wakifanya kila kitu kufanisi na kiufasaha.
Mpaka mapumziko Simba walikuwa mbele kwa bao 2-1.
Simba walirejea tena kwa kasi ile ile ya kipindi cha kwanza wakionekana kuongeza kucheza kwa mipango zaidi.
Vivian Corazone aliipatia timu yake ya Simba Queens bao la 3 dakika ya 49 baada ya Fatuma Issa kugongeana tena vizuri na Elizabeth Wambui kwenye mpira wa adhabu ambaye naye akapiga krosi iliyomkuta mfungaji. Pasi ya usaidizi ya 3 kwa Elizabeth Wambui. Simba Queens 3-1 Yanga Princess.
Yanga walimtambulisha mchezoni mchezaji wao mpya mwenye asili ya Ulaya, Wilson. Huku Simba Queens nao wakifanya mabadiliko kwa kuwaingiza Diana Mnaly, Esther Mayala na Issabelle Diakise wakipumzishwa Fatuma Issa, Asha Djafar na Danai Bhobho.
Simba Queens kwenye mchezo wa leo ukiacha tu kuwa bora kwenye maeneo mengi kwenye uwanja walifanikiwa pia zaidi kumnyima nafasi ya uhuru Precious Christopher ambaye ndiye mchezaji hatari zaidi wa Yanga Princess.
Dakika ya 84, Aisha Mnunka alipata majeraha na nafasi yake kuchukuliwa na Olaiya Barakat lakini akiingia pia Koku Kipanga nafasi ya Ritticia Nabbosa. Lakini Faiza Seidou aliingia nafasi ya Precious Christopher kwa upande wa Yanga Princess.
Simba waliendelea kuwa timamu mpaka dakika zote 90 zilipomalizika na kuhakikisha wanaibuka na alam zote 3. Simba Queens 3-1 Yanga Princess.
Huu ni mchezo wa 8 sasa Simba wanaifunga Yanga kwenye michezo 13 waliyokutana huku Yanga Princess wakishinda mchezo 1 tu pekee.