Klabu ya Young Africans hii leo imeingia mkataba na shirika la Bima la NIC wenye thamani ya TZS Million 900, mkataba huu utakuwa wa miaka mitatu wenye kipengele cha kutoa tuzo ya mchezaji bora wa kila mwezi wa klabu. Mchezaji bora wa klabu ya Young Africans atakuwa anapigiwa kura na mashabiki wa klabu hiyo kila mwezi.
akizungumza katika hafla ya utiaji saini iliyofanyika leo Serena Hotel Rais wa klabu hiyo Eng. Hersi Said amesema mkataba huu utaenda kuinufaisha klabu ya Yanga kwa asilimia kubwa na utaongeza ushindani kwenye kikosi chao kutokana na uwepo wa tuzo za mchezaji bora wa mwezi.
Makubaliano haya yanakwenda kumnufaisha mchezaji bora atakayekuwa anapatikana kila mwezi, Young Africans itaenda kunufaika na mkataba huu ambao ni mkataba wa miaka mitatu, itanufaika kimapato kwa kiasi cha million mia tisa (900 M).
Eng. Hersi Said Rais wa klabu ya Young Africans.
Hersi pia amesema miongoni mwa sababu zilizowavutia NIC kuwekeza ndani ya klabu ya Young Africans ni uwepo wa wachezaji bora kwenye kikosi hicho ambao yeye anaamini hawawezi kupatikana kwenye klabu yoyote ile.
Tunaelewa kwanini NIC wamechagua kufanya kazi na sisi. Tuna wachezaji bora zaidi ambao huwezi kuwapata kwenye klabu nyingine. Wachezaji hawa wana ushawishi mkubwa nje na ndani ya uwanja. Ushawishi wao ni chachu ya kutangaza biashara hii ya BIMA.
Eng. Hersi Said wakati wa hafla ya utiaji saini.
Kwa upande wa Elihuruma Doriye ambaye ni mtendaji mkuu wa shirika la Bima la NIC wakati wa hafla hiyo amesema Young Africans ndio nembo ya soka kwa Tanzania akiwa bingwa wa kihistoria.
Leo historia imeandikwa baada ya taasisi mbili zenye chapa ya kihistoria kwa Tanzania kuingia makubaliano ya kibiashara kwa miaka mitatu. Huwezi kuzungumzia BIMA bila kuitaja NIC, na katika soka Young Africans ndio nembo ya soka kwa Tanzania akiwa bingwa wa kihistoria. Tunayo furaha kubwa kupata fursa ya kufanya biashara na taasisi kubwa kama hii. Kwa upande wetu NIC imepewa hadhi ya kuaminika kama taasisi inayotoa huduma kwa weledi mkubwa. Wananchi, BIMA ni NIC.