Connect with us

PBZ Premier League

ZANZIBAR INA VIPAJI, KWANINI LIGI NI DHAIFU?.

Zanzibar ni moja kati ya maeneo mengi nchini Tanzania ambayo yanasifika kuwa na wachezaji nyota ambao hufunzwa soka tangu wakiwa vijana wadogo hadi wanapokuwa wakubwa.

Mifano ipi mingi, akiwemo mwanasoka wa zamani wa Yanga na timu ya Taifa ya Tanzania Abdi Kassim Babi, Nyota anayeitumikia Azam kwasasa Feisal Salum, Mudathir Yahya, Maabadi Maulid Maabad anayeitumikia Coastal Union na wengine wengi.

Licha ya sifa zote hizo kutoka kwenye kisiwa cha karafuu, lakini bado Ligi yao imekuwa haina mvuto mkubwa kama zilivyo Ligi zingine ikiwemo Ligi kuu kandanda Tanzania Bara.

Ally Mohamed ni Afisa habari wa klabu ya Mlandege ambayo imekuwa na mafanikio makubwa kwenye mashindano ya Mapinduzi Cup kwa misimi hii miwili ikifika fainali [2023 – Bingwa, 2024 – Fainali vs Simba], yeye ameeleza sababu kadhaa zinazopelekea Ligi ya Zanzibar kukosa mvuto.

  • Timu hazina maandalizi ya kutosha.

Tmu nyingi kutoka visiwani Zanzibar hazina utaratibu wa kuweka kambi, mara nyingi huweka kambi siku ya mchezo husika.

“Ukiangalia kwa Bara timu zinaweka kambi kwa muda mrefu lakini huku kwetu Zanzibar timu zinaweka kambi siku ya mchezo”.

“Wanaweza kukutana saa nne asubuhi hadi muda wa mchezo na baada ya hapo kila mmoja anasambaa anaendelea na kazi zake”, alisema Ally Mohamed.

Miundo mbinu

Kabla ya ujenzi wa uwanja wa New Amaan Complex ni viwanja viwili tu ambavyo vinatumika kwaajili ya michezo yote ya Ligi kuu Zanzibar kitu kinachopoteza ladha ya mpira.

“Kabla ya uwanja wa New Amaan tulikuwa na viwanja viwili, uwanja wa finya [Pemba] na Mao [Unguja], kiuhalisia ni uwanja ambao unatumika kwenye Ligi lakini ukifuata mahitaji ya uwanja unaona vina mapungufu makubwa”. Alisema Ally.

  • Umbali

Ally Mohamed anasema mara nyingi timu inasafiri kwa takribani saa kumi [10] na wanakuwa na muda mchache wa kupumzika hivyo ushindani unakuwa mdogo.

“Ukicheza mechi mbili [2] kwa Unguja, utacheza na klabu ambazo ziko Unguja, ukicheza ugenini kwa klabu ambazo ziko unguja, utacheza hapo hapo uwanja wa Mau”.

“Ukicheza na klabu za Pemba lazima usafiri, na ni umbali mrefu sana na usafiri tunaoutumia ni wa majini, ni takribani masaa nane unakaa kwenye maji kuifuata timu”.

“Tunachukua saa takribani 10, kwenye maji nane na barabarani mbili kuifuata timu, ukifika hapo pengine una siku moja tu, kwa kiasi fulani ufanisi unakosekana”, Ally aliongeza.

  • Uchumi

Timu nyingi hazina wadhamini wao binafsi kitu ambacho kina wafanya watumie pesa nyingi sana na wakati mwingine wanashindwa kutimiza baadhi ya vitu mhimu ikiwemo usajili wa nyota wakubwa kama ilivyo kwa Ligi zingine.

“Mdhamini sio kila kitu, klabu katika swala la uendeshaji, fedha wanazozipata kutoka kwa hawa wadhamini zinaweza kumalizika kabla hata nusu ya msimu haijakamilika”, aliongeza Ally.

Mashabiki wa soka visiwani Zanzibar bado hawaamini katika kile kinachotolewa na klabu zao za nyumbani na asilimia kubwa ya watu hapa ni mashabiki wa timu za Tanzania Bara [Simba na Yanga].

“Hapa kwetu vipaji vipo lakini Ligi yetu haichezwi kama ilivyo kwa Tanzania Bara, na hata zingeingia timu za hapa kwetu fainali ya mapinduzi ungeona mashabiki wachache uwanjani, huku kwetu hakuna ushindani” Alisema shabiki mmoja.

Ligi yoyote ili iweze kufanikiwa kwa kiasi kikubwa lazima kuwe na uwekezaji mkubwa kutoka kwa wadhamini pamoja na klabu zenyewe, kwa maeneo ya Zanzibar asilimia kubwa ya watu wanapenda sana kuangalia mpira.

Makala Nyingine

More in PBZ Premier League