Kocha mkuu wa muda wa kikosi cha Ivory Coast Emerse Fae alikuwa miongoni mwa nyota walioiwakilisha timu ya Taifa ya Ivory Coast mwaka 2006 wakati wakipoteza mchezo wa fainali dhidi ya Misri kwa mikwaju ya penalty, 4-2, fainali zilizopigwa pale pale Misri.
Kwenye mchezo ule akiwa amevalia jezi yake namba 7 mgongoni alikichafua dakika zote 120, lakini penalty hakupiga, lakini wakanyimwa ubingwa na Didier Drogba aliyekosa penalty na Bakari Kone [Aliyeingia kuchukua nafasi ya Yaya Toure].
Mwana anaona bado ana deni anadaiwa na Taifa lake, kile alichoshindwa kukifanya mwaka 2006 akiwa mchezaji pengine anatamani akifanye 2024 akiwa kocha wa muda tena kwenye ardhi yake ya nyumbani.
Ivory Coast ilikuwa imebadilika sana kwenye game dhidi ya Senegal, ni tofauti na Ivory Coast iliyokipiga dhidi ya Equatorial Guinea kabisa.
Fae ameshinda vita ya wazawa mbele ya mbabe kutoka Senegal Legend huyu Aliou Cisse.
Fae amezaliwa Ufaransa, amecheza timu za vijana za Ufaransa na baadae akachagua kuitumikia timu ya wakubwa ya Ivory Coast.
Ameitumikia timu ya Taifa ya Ivory Coast kwenye michezo 41 akicheza nafasi ya kiungo mshambuliaji na kufunga goli moja [1] pekee.
Amewahi kucheza klabu za Nantes [Ufaransa], Reading [England] na Nice [Ufaransa]. Amecheza takribani michezo 203 na kufunga magoli takribani 17.
Katika kipindi ambacho Ivory Coast wanajiuliza tunaendaje kwenye mechi dhidi ya bingwa mtetezi mwana akatokeza na kusema nitumeni mimi, wamemtuma karudi na kitoweo.
Tuendelee kuwekeza kwa wachezaji wa zamani wa timu yetu ya Taifa ya Tanzania pengine linaweza kuwa msaada mkubwa hapo baadae maana asilimia kubwa ya makocha wanaofanya vyema kwenye timu za Taifa ni wazawa.