Mwinyi Zahera na vijana wake bado wanajitafuta huku wakizidi kujichimbia kaburi lao wenyewe kwenye Msimamo wa ligi kuu wakiendelea kusalia nafasi yao ya 15 wakiwa na alama 3 tu pekee kwenye michezo 6 waliyocheza hadi sasa.
Mpira ulionekana kuwa na kasi dakika 10 za mwanzo lakini bado hapakuonekana timu iliyokuwa makini kwenye kutengeneza nafasi na kuzitumia. Dakika ya 8 Mubarak Hamza Ngamchiya alipiga shuti kali la chini chini lakini lilienda kando ya lango.
Ihefu waliendelea kulisakama goli la Coastal Union na dakika 21 Rashid Juma Mtabwigwa alikimbia na mpira pembeni na kupiga krosi nzuri lakini haikuwa na mmaliziaji na kuishia kwenye mikono ya golikipa Alaine Matampi alikuwa kwenye kiwango bora sana hii leo.
Dakika ya 40 kipindi cha kwanza Charles Ilanfya alijitengenezea nafasi na kupiga shuti kali la chini na kwa mara nyingine na golikipa Matampi alikaa vizuri. Mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika Ihefu 0-0 Coastal Union.
Ni kama Coastal walikuwa wanazurula uwanjani, kwani golikipa wa Ihefu, Fikirini Bakari hakuhitaji kufanya uokoaji hata mmoja. Ihefu walirudi tena kwa nguvu kipindi cha pili kwa kuwasakama Coastal langoni kwao, safari hii waliamua kufanya ulinzi kwa kurudi nyuma.
Dakika ya 71, Ibrahim Ajibu alipata nafasi kupitia mpira wa adhabu ndogo nje kidogo ya goli lakini mpira wake uliwababatiza walinzi wa Ihefu na kuokolewa. Hapakuwa na matukio mengi ya kuripoti kwenye mchezo huu mpaka dakika ya 87 Ihefu walipata nafasi nyingine ya kupata bao la ushindi lakini nyota wa mchezo huu wa leo, Matampi aliwaweka salama tena wageni.
Mpaka filimbi ya mwisho ya mwamuzi Raphael Ikambi inapulizwa, mchezo ukamalizika kwa 0-0 kwa timu zote mbili kutoka na alama moja moja huku Coastal Union wakitoka bila shuti hata moja lililolenga lango na moja pekee likiwa halijalenga goli.