Connect with us

NBC Premier League

YANGA MBELE KWA MBELE

Yanga wanapata ushindi wa pili mfululizo kwenye dimba la Benjamin Mkapa kwa kuwachapa Singida FG mabao 2-0 na kuendelea kujikita kileleni mwa msimamo kwa kufikisha alama 18 baada ya michezo 7 ya ligi ya NBC msimu huu.

Singida FG, walianza mchezo kwa kujihami, wakicheza chini kabisa huku wakijaribu kushambulia kwa kushitukiza. Mchezo huu ulikuwa hatari sana kwao kwani kuruhusu Yanga kucheza hasa kwenye eneo lao kulizidisha Yanga kujiamini na kutengeneza mashambulizi mengi. Viungo wote watatu washambuliaji wa Singida FG, Bruno Gomes, Duke Abuya na Marouf Tchakei walishuka chini na kusababisha msongamano. Ni rahisi kufanya makosa. 4-2-3-1 hugeuka na kuwa 4-5-1 kwa kipindi hiki.

Yanga walitumia hii kwa faida yao, Ilifanya Mauya na Mudathir kuongezeka kwenye kufanya mashambulizi kusaidia viungo watatu wa juu, Maxi, Aziz Ki na Pacome, maana yake ilikuwa kwamba kuna mchezaji mmoja alikuwa Huru kila wakati Yanga wakifanya Mashambulizi.

Dakika ya 16 ya mchezo, Singida FG walifanya makosa ya kimawasiliano ya kiulinzi na golikipa Benedict Haule kujikuta anawazawadia Yanga nafasi lakini hata hivyo Hafiz Konkoni hakuweza kutumia nafasi hiyo kwa kummlenga golikipa Haule.

Mchezo uliendelea kuwa wa upande mmoja muda mwingi licha ya nafasi chache walizozitengeneza, dakka ya 27, Pacome Zouzoua anapata nafasi ya wazi ya kuipatia goli la kutangulia timu yake, lakini shuti lake likammlenga Haule kwa mara nyingine.

Duke Abuya anapata kadi ya njano dakika ya 28 kwa kuonyesha utovu wa nidhamu.

Dakika ya 30, Maxi Nzengeli anaipatia Yanga goli la kwanza kwa kuunganisha krosi ya Yao Kouasi kwa kichwa mbele ya Biermes Carno, mpira ukimmshinda Haule ambaye pia alijaribu kutokea kucheza krosi hiyo. 1-0 Yanga.

Dakika ya 38, Maxi Nzengeli tena anawanyanyua wananchi vitini kwa kufunga bao la pili kwake na la pili kwa timu yake. Pacome Zouzoua anakimbia na mpira na kummpa pasi Maxi ambaye anajitengenezea nafasi na kupiga shuti kali lililomshinda tena golikipa Haule. 2-0 Yanga.

Benedict Haule anashindwa kuendelea na mchezo na kufanyiwa mabadiliko na kuingia Rashidi Parapanda dakika ya 40.

Yanga bado waliendelea kuutawala mchezo mpaka dakika 45 zinakamilika. Mapumziko Yanga anatoka kifua mbele kwa 2-0.

Kipindi cha pili timu zote zinaingia na mbadiliko, Yanga wakimuingiza Salum Abubakar “Sure Boy” badala ya Mudathir Yahya na Singida FG wakimuingiza Deus Kaseke na kummtoa Habibu Kyombo na Kumuingiza Francy Kazadi badala ya Duke Abuya.

Dakika ya 48, Yao Kouassi alimmpa pasi nzuri ya kumalizia tu(tap in) Hafiz Konkoni lakini alipaisha.

Deus Kaseke anaonyeshwa kadi ya njano, dakika yake ya 4 tu mchezo baada ya kummchezea vibaya Dickson Job.

Singida FG walijitengenezea nafasi kupitia mpira wa kutenga wa Bruno Gomes, na almanusura Makame aipatie Bao timu yake kutokana na krosi hii lakini alishindwa kuimalizia. Dakika ya 55, Yusuf kagoma alionyeshwa kadi ya njano kwa kummchezea vibaya Stephane Aziz Ki wakati wakijibu shambulizi. Kadi ya 3 ya njano kwa Singida FG. Muda huo huo, Bruno Gomes anatoka na kummpisha Morice Chukwu kwenda kuongeza nguvu ya kiungo cha ulinzi.

Marouf Tchakei anafanyiwa madhambi nje kidogo ya eneo la goli la Yanga na Yao Kouassi. Lakini pigo lake linakuwa halina manufaa kwa timu yake kwa mpira kupaa juu ya lango la Diarra. Bado Singida hawajaweza kunufaika na mipira hii ya kutenga. 2-0 bado dakika ya 60.

Dakika ya 62, Stephane Aziz Ki anaukwamisha mpira nyavuni lakini anahukumiwa na kibendera cah Muamuzi msaidizi kuwa alikuwa ameotea wakati anapokea pasi kutoka kwa Yao Kouassi.

Biemes Carno anaonyeshwa kadi ya njano kwa kumchezea faulo Aziz Ki wakati akielekea lango la Singida FG. Carno anacheza faulo ya kiufundi. Kadi kwa ajili ya timu.

Dakika ya 72, Mabadiliko yanafanyika kwa timu zote mbili, Yanga wanawapumzisha Hafiz Konkoni na Kuingia Mahthlase Makudubela “Skudu” lakini pia akitoka Pacome Zouzoua  na Kuingia Kennedy Musonda. Singida FG wao wakimmtoa Azizi Andabwile na kumuingiza Mshambuliaji Meddie Kagere, mfumo kubadilika na kuwa 4-4-2.

Dakika ya 76, Yanga walifanya mabadiliko mengine wakimmpumzisha Lomalisa Mutambala na kumuingiza Nickson Kibabage. Dakika ya 79, Kibabage alipata nafasi nzuri ndani ya eneo la Singida FG akigongeana pasi vizuri na Skudu lakini shuti lake likaokolewa na Parapanda. Singida FG wanapata kadi ya Njano ya Mchezo dakika ya 80 baada ya Yahya Mbegu kufanya madhambi.

Yanga walicheza dakika 10 bila ya kuwa na mshambuliaji asilia, dakika ya 83 akatoka kiungo Aziz Ki  na kuingia mashambuliaji Clement Mzize. Kennedy Musonda akasogea winga ya Kulia kummpisha Mzize kama mshambuliaji wa kati.

Singida FG bado walionekana kutokuwa na madhara kabisa mbele ya lango la Yanga. Wakiwa hawajapiga hata shuti moja lililolenga lango kipindi hiki cha pili. Dakika 4 zinaongezwa kumalizia dakika 90 lakini ni kama dakika zote walipewa Yanga wacheze.

Mpira unamalizika na Yanga wanaibuka na ushindi wa 2-0.

Makala Nyingine

More in NBC Premier League