Connect with us

NBC Premier League

TATHMINI MICHEZO YA LEO LIGI KUU YA NBC

JKT TANZANIA V DODOMA JIJI

AZAM COMPLEX, DAR ES SALAAM

SAA 10.00 JIONI

Timu zote mbili zinaingia na kumbukumbu ya kupata matokeo mazuri kwenye michezo yao iliyopita. JKT TANZANIA wakimmfunga 1-0 Tabora United na Vijana wa Melis Medo wakipata ushindi wa 1-0 dhidi ya Kagera Sugar.

JKT wapo nafasi ya 5 wakiwa na alama zao 11 baada ya michezo 7, alama 1 tu nyuma ya KMC nje ya nafasi 4 za juu ambazo ndio malengo haswa ya timu msimu huu kwa mujibu wa George Mketo, kocha msaidizi. Wanatambua ushindi wa leo nyumbani ni muhimu sana kuelekea kutimiza malengo yao taratibu kwani alama 3 leo, zitawapandisha mpaka nafasi ya 3 wakimmshusha Azam Fc.

Hali sio mbaya kwa Dodoma pia, kwani wanayo nafasi ya kummsogelea KMC pia kama watashinda leo. Alama zao 9(2 tu nyuma JKT), baada ya michezo 7 imewafanya wawe nafasi ya 6, nyuma ya wapinzani wao wa leo. Bila kujali malengo yao, hata wao wanazitaka kwelikweli alama 3 za leo.

TANZANIA PRISONS V GEITA GOLD

SOKOINE STADIUM, MBEYA

SAA 10.00 JIONI

Vita kubwa hii ya makocha wazawa wenye wasifu mkubwa sana nchini, lakini inachochewa zaidi na nafasi walizopo kwenye msimamo wa ligi kuu msimu huu.

Fred Minziro na vijana wake wametoka kupata sare dhidi ya KMC ya 1-1, wakifikisha alama 6 wanashika nafasi ya 14, huku Hemed Moroco na vijana wake wanaburuza mkia na alama zao 5 baada ya michezo 7. Wote wapo kwenye nafasi za hatari na wanatamani kujinasua huko. Vita sio nyepesi hii.

Tanzania Prisons wana uwezo wa kupanda hadi nafasi ya 8 kama watashinda mchezo wa leo wakiombea Tabora apoteze lakini Geita Gold wanaweza kujinasua hadi nafasi ya 11. Ushindi ni muhimu na lazima  kwa timu zote mbili.

KAGERA SUGAR V TABORA UNITED

KAITABA STADIUM, KAGERA

SAA 1.00 JIONI

Mecky amefanikiwa kukusanya vipaji vingi sana kwenye timu yake lakini ameshindwa  kuwa na muendelezo wa matokeo mazuri kwenye msimu huu. Wametoka kupoteza 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji ugenini, licha kucheza vizuri lakini bado matokeo mfululizo yamekuwa ya kusua.

Goran Kopunovic atahitaji kusahau haraka sana kiwango cha mchezo uliopita na kuingia na maboresho makubwa kwenye mchezo wa leo. Hakuwa na mchezo mzuri dhidi ya JKT Tanzania akipoteza 1-0 lakini timu kutocheza vizuri pia. Anahitaji kuwa vizuri leo dhidi ya timu yenye kutaka kurejesha makali yake wakiwa nyumbani.

Wakiwa wamepishana nafasi 2 na alama 1 tu, Kila mtu anaona mwanya wa kummtambuka mwenzie ndio huu. Yoyote atakayeshinda leo ana nafasi ya kuingia 5 bora kwenye msimamo kutoka nafasi walizopo sasa(9 –Kagera Sugar na 7- Tabora United). Waswahili wanasema, Kitaumana.

Makala Nyingine

More in NBC Premier League