Connect with us

NBC Premier League

TATHMINI YA MICHEZO YA LEO LIGI KUU YA NBC

SINGIDA BIG STARS V IHEFU

LITI STADIUM, SINGIDA

SAA 8.00 MCHANA

Singida Big Stars wanatoka kwenye kupoteza mchezo wao dhidi ya Yanga kwa 2-0, wanarejea nyumbani kwenye uwanja wao wa Liti kukabiliana na Ihefu ambao pia wametoka kupoteza 2-1 dhidi ya Simba.

Wote wanatafuta ushindi wao wa 3 msimu huu na hawajawa na msimu bora hadi hivi sasa, Singida wakiwa nafasi ya 10 na alama zao 8, Ihefu wakiwa nafasi ya 11 na alama 7.

Ushindi wa Singida Bs utawasogeza hadi nafasi ya 7 huku kama Ihefu watashinda basi watasogea hadi nafasi ya 8.

Mchezo mzuri sana kuutazama na wenye upinzani wa hali ya juu kutokana na ubora wa vikosi vyao, ni vile hawapati matokeo tu na leo ni siku kubwa sana kwa timu zote mbili.

MASHUJAA V AZAM FC

LAKE TANGANYIKA, KIGOMA

SAA 10.00 JIONI

Uwanja wa Lake Tanganyika umekuwa na matokeo mazuri kwa timu ya Mashujaa, wakirekodi ushindi mara 2 kwenye uwanja huo. Lakini hawajawa na matokeo mazuri nje ya uwanja wao ila leo wanarejea hapo kukabiliana na Azam FC.

Wote wawili wametoka kupigika, Mashuja akifungwa na Coastal Union 2-0 na Azam akifungwa kwao 3-1 na Namungo. Haitokuwa mechi rahisi kwa timu zote kwani vipigo ni kama vimewavurugia dira yao. Ushindi wa leo ni muhimu kwa timu zote.

Mashujaa wanashika nafasi ya 9, wakiwa na alama 8 baada ya michezo 6 na wana nafasi ya kusogea hadi nafasi ya 7 wakishinda huku Azam wakiwa nafasi ya 4 wakiwa na alama 13 baada ya michezo 7 na wana uwezo wa kupanda hadi nafasi ya 3 wakishinda mchezo huu.

Hatumwi  mtu dukani, Sokwe anaitamani Ice Cream.

COASTAL UNION V NAMUNGO

CCM MKWAKWANI, TANGA

SAA 1.00 JIONI

Kabla ya raundi 7, Coastal Union na Namungo walikuwa hawajarekodi ushindi hata mmoja, lakini mbele ya timu ngumu za Azam FC na Mashujaa timu zote mbili zikapata ushindi wao wa kwanza msimu huu. Coastal Union akimmfunga Mahujaa 2-0 na Namungoa akimmfunga Azam 3-1.

Mchezo wa leo wote watatamani kuendeleza wimbi la ushindi ili kujiongezea kujiamini kwenye michezo inayokuja. Wakiwa wamefanana takribani kila kitu kwenye mechi zao 7(W1, L3, D3) na wamepishana kwa nafasi 1 tu, nyasi za uwanja wa Mkwakwani zitakuwa kwenye tafrani wanaume hawa wakipambania alama 3.

Wagosi wa Kaya wanashika nafasi ya 14 wakiwa na alama 6 baada ya michezo 7 na Namungo wakiwa nafasi ya 13, wakiwa na alama 6 pia. Kuna uwezekano wa mmoja wao kufika hadi nafasi ya 9 hii leo.

Makala Nyingine

More in NBC Premier League