Mchezaji wa Arsenal, Declan Rice ameelezwa kuongezea uhatari zaidi kwenye safu ya ushambuliaji ya timu yake tofauti na ilivyodhaniwa.
Rice, 24, amefunga mabao 2 na kutoa pasi za usaidizi 3 mpaka hivi sasa kwa Arsenal akitokea kwenye nafasi yake ya kiungo mkabaji. Ikiwa leo wanakutana na timu yake ya zamani West Ham akisajiliwa kwa Pauni Milioni 105, anatarajiwa kuwa mchezaji muhimu kwenye safu ya kiungo kwani amekuwa hivyo msimu huu tangu asajiliwe.
Kwenye michezo mitatu ya mwisho dhidi ya Chelsea, alifunga goli muhimu la kuirejesha timu yake mchezoni kabla ya kwenda kusawazisha na matoke kuwa 2-2 lakini kwenye ushindi wa 2-1 kwenye Ligi ya mabingwa itakumbukwa pasi yake maridadi kwa Gabriel Jesus kufunga kabla ya kuatoa tena pasi ya Usaidizi kwa Eddie Nketiah kufunga moja ya mabao yake matatu kwenye ushindi wa 3-0 dhidi ya Seffield United.
Hakuna mchezaji wa Arsenal aliyeshinda mipira mingi ya kugombania zaidi yake, lakini uwezo wake wa kupasia na kufunga pia ni kama ziada kwa timu yake na inasaidia sana. Alipoulizwa kocha wake Mikel Arteta juu ya uwezo wa mchezaji wake huyo mpya alisema
Declan ni mchezaji mzuri sana na nafahamu uwezo wake. Amekuwa na msaada mkubwa kwenye eneo la kiungo na hilo ndilo unalotamani kuliona kwa wachezaji wako wakubwa, lakini kuona anaongezea na uwezo wa kufunga na kupasia inafurahisha zaidi na huu ni ukuaji.