Connect with us

NBC Premier League

YANGA YAISAMBARATISHA SIMBA

Yanga wameisambaratisha vibaya Simba hii leo kwa kuwanyuka mabao 5-1 katika mchezo ambao ulikuwa na nyakati na vipindi tofauti kwa timu zote mbili, lakini ni Yanga ndio waliokuwa na cheko la mwisho, wakipata ushindi muhimu mbele ya wapinzani wao kwenye kuwania ubingwa, wakirejea kileleni mwa msimamo wakifikisha alama 21 baada ya michezo 8.

Mpira ulianza kwa kasi kwa timu zote mbili lakini dakika ya 3 tu ya mchezo, Yanga walionyesha kuutaka mchezo na walitangulia kupata goli la uongozi kupitia kwa Kennedy Musonda akifunga kwa kichwa akiunganisha krosi maridadi kutoka kwa Yao Kouassi kutokea upande wa kulia wa Yanga, wakati walinzi wa Simba wakishindwa kufanya majukumu yao vizuri. 1-0 Yanga.

Dickson Job alichukua kadi kwa ajili ya timu akiokoa shambulizi la hatari baada ya Saido Ntibazonkiza kupokea mpira ambao uliopigwa vibaya na Djigui Diarra na wakati Saidoo akiwa analielekea lango la Yanga, alikwatulia na Job. Faulo na kadi ya njano kwake, dakika ya 8 ya mchezo.

Clatous Chama alipiga pigo lililookolewa vizuri kabisa na Diarra, na kuwa kona

Dakika ya 10 ya mchezo, Kibu Denis anawasawazishia Simba kwa kichwa kutokana na kona iliyosababishwa na kuokolewa kwa pigo la faulo la Clatous Chama. Kona ikichongwa na Saidi Ntibazonkiza na Kibu Denis akaunganisha kwa kichwa. 1-1.

Aishi Manula anafanya kosa linalosababisha Ngoma kucheza faulo kuinusuru timu yake na kupewa kadi ya njano dakika ya 23, hata hivyo pigo la Azizi Ki libabatiza ukuta na mpira kuwa kona ambayo haikuwa na madhara kwa Simba.

Mchezo uliendelea lakini ukiwa wa kusikiliziana, Yanga wakijenga zaidi mashambulizi lakini Simba nao wakijibu. Dakika ya 41, ilimmlazimu Aishi kuokoa mashuti mawili yaliolekezwa kwake, kutoka kwa Azizi Ki na Pacome Zouzoua na kuliweka lango la Simba Salama. Shambulizi la hatari walifanya Yanga dakika hizi.

Mapumziko timu zote zilitoshana nguvu kwa kufungana 1-1.

Hakuna mwalimu aliyefanya mabadiliko kipindi cha pili, na mechi ilirejea na kasi yake ya kipindi cha kwanza. Alamnusura Simba wapate goli mapema lakini Jean Baleke alikosa utulivu mbele ya mabeki wa Yanga na kukosa nafasi ya kuandika bao.

Simba wanapata nafasi nje kidogo ya eneo la Yanga kwa adhabu ya pigo kubwa. Saido pigo lake lilipaa juu ya lango. Dakika hizi pia Kibu Denis alichezewa faulo na Diarra iliyommfanya ashindwe kuendelea na mchezo.

Dakika ya 58, Jean Baleke alitengewa pasi nzuri na Saidio Ntibazonkiza na kuachia shuti kali lililoenda kugonga nguzo ya juu ya lango la Yanga. Luis Miquissone anaingia nafasi ya Kibu Denis.

Dakika ya 63, Yanga walipata bao la pili wakitumia nafasi ya Simba kufanya uzembe wakati wanashambulia na kupoteza mpira uliommkuta Stephan Aziz Ki aliyepiga pasi elekezi kwa Maxi Nzengeli ambaye kasi yake iliwazidi mabeki wa Simba na kupiga shuti la chini lililommshinda Aishi Manula. 2-1 Yanga.

Simba waliendelea kufanya makosa hasa ya kiulinzi na wakichelewa kufika kwenye njia za Yanga hali iliyopeleka hatari nyingi sana golini kwao. Maxi Nzengeli alipiga shuti kali lililopanguliwa vizuri na Aishi Manula dakika ya 68 ya mchezo.

Simba wanammtoa Jean Baleke na kumuingiza Moses Phiri, na Yanga nao wakimuingiza Clement Mzize nafasi ya Kennedy Musonda.

Dakika ya 74, Stephane Azizi Ki alifunga bao la 3 kwa Yanga na bao lake la 7 msimu huu. Akipokea pasi nzuri kutoka kwa Clement Mzize baada ya kazi nzuri ya kulazimisha ya Pacome Zouzoua. Azizi Ki bado ilimmlazimu kufanya kazi ya ziada kuwashinda mabeki wa Simba na kufunga.3-1 Yanga.

Hali iliendelea kuwa mbaya kwa Simba wakizidi kufanya makosa ya kiulinzi. Wakishindwa kufanya uzuiaji kuanzia juu na kupoteza mipira. Dakika ya 76, Yanga wanaandika bao la 4, akifunga Maxi Nzengeli goli lake la pili hii leo akipokea pasi safi kutoka kwa Clement Mzize. 4-1 kwa Yanga.

Almanusura Yanga wafunge bao la 5,dakika ya 83, Pacome Zouzoua alipokea pasi kutoka kwa Azizi Ki akiwa anaangaliana na Aishi Manula, alipiga shuti lililopaa juu ya lango. Mudathir Yahya anatolewa na kuingia Jonas Mkude.

Yanga wanapata penati dakika ya 86 baada Henock Inonga kummfanyia madhambi Maxi Nzengeli na Pacome Zouzoua hakufanya ajizi. Akimmpeleka Markiti Aishi Manula. 5-1 Yanga.

Dakika ya 88, Yanga walifanya Mabadiliko matatu kwa mpigo, wakimuingiza Skudu, Kibabage na Birthday boy, Mwamnyeto.

Simba walikuwa wametota kabisa. Wakiendelea kufanya makosa. Haikuwa siku njema kwao. Pengine watatamani siku ya leo waisahau haraka. Wangeweza kuadhibiwa zaidi kama Yanga wangeendelea kutumia nafasi zao au wangeongeza kasi kama waliyokuwa nayo.

Simba walipoteana zaidi eneo la kiungo, wakiwaruhusu Yanga kufanya wanvyotaka. Utasifu akili ya Gamondi kuamua kuongeza viungo na kuamua kuutoa mpira pembeni na kuiingiza katikati ya kiwanja. Mapana hayakutumika sana, bali mchezo ukapelekwa kwa Azizi Ki, Nzengeli na Pacome huku Mzize akicheza chini sio kama mshambuliaji, hii ilimaanisha yoyote angeweza kufunga na kila nafasi waliyoipata waliitumia vizuri.

Dakika 90 zinamalazika na kipyenga cha Ahmed Aragija kinahitimisha Derby ya Kariakoo, Yanga wakishinda 5-1. Simba wanapoteza mchezo wa kwanza msimu huu.

Makala Nyingine

More in NBC Premier League