Connect with us

FIFA World Cup

STARS YAICHAPA NIGER UGENINI LEO.

Timu ya Taifa ya Tanzania imevuna alama tatu (3) ugenini dhidi ya timu ya Taifa ya Niger, mchezo uliopigwa katika uwanja wa Grand Marrakech Annex nchini Morocco.

Mchezo huu umechezwa Morocco kwasababu Niger haina uwanja unaokidhi kuchezewa michezo ya kufuzu fainali za kombe la Dunia hivyo wakachagua kutumia uwanja wa Grand Marrakech Annex uliopo nchini Morocco.

Kwenye mchezo huo zilitokea kosakosa nyingi ikiwemo ile iliyotokea dakika ya 36 ya mchezo baada ya nahodha wa kikosi cha Stars Mbwana Ally Samatta kupiga Faulo iliyoenda kugonga mwamba na kurudi uwanjani.

Stars haikukoma kuliandama lango la Niger licha ya kuanza na viungo wengi wa ulinzi kuliko wa ushambuliaji na kosakosa zilikuwa nyingi lakini hadi dakika 45 zinamalizika hakuna timu iliyokuwa imefanikiwa kuliona lango la mwenzake.

Kipindi cha pili cha mchezo kilipoanza Stars iliendelea kuliandama lango la Niger na hatimae dakika ya 56 Stars iliandika goli kupitia kwa kiungo wake mshambuliaji Charles M’mombwa aliyepiga shuti kali ndani ya eneo la 18 lililombabatiza beki wa Niger na kumuacha golikipa akiwa hana cha kufanya.

Hili linakuwa goli la kwanza kwa kijana Charles M’mombwa ambaye ni kwa mara ya kwanza anavaa jezi ya timu ya Taifa na kulitumikia Taifa lake katika michezo ya mashindano.

Benchi la Adel Amrouche lilifanya mabadiliko dakika ya 67 kwa kumtoa mfungaji wa goli pekee la Stars Charles M’mombwa na kumtambulisha mchezoni Kibu Denis Prosper.

Baada ya mabadiliko hayo Stars waliendelea kulisakama lango la Niger na kukosa nafasi kadhaa ikowemo ile aliyokosa nahodha Mbwana Samatta akiwa yeye na golikipa wa Niger.

Haikuishia hapo Haji Mnoga pia alikosa kuiandikia goli la pili Stars baada ya kuupiga nje mpira uliotemwa na golikipa wa Niger.

Dakika ya 75 ya mchezo Kocha Adel Amrouch anamtambulisha mchezoni kiungo fundi Himid Mao Mkami na kumpumzisha nyota Feisal Salum.

Dakika ya 90 ya mchezo Dickson Job anaumia wakati anagombea mpira na mchezaji wa Niger na kutewa nje huku nafasi yake ikichukuliwa na Morice Abraham.

Morice alikuja kuongeza kasi kwenye eneo la kiungo cha Taifa Stars na hadi mpira unamalizika Stars ilikuwa inaongoza goli 0-1 dhidi ya Niger.

Mchezo unaofuata kwa Tanzania ni dhidi ya Morocco, utakaopigwa Jumanne ya November 21 katika uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar Es Salaam.

Stars sasa ipo nafasi ya pili ya msimamo wa kundi E nyuma ya Zambia ikiwa na tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa baada ya Zambia kuichapa Congo Brazzaville goli 4-2 hapo Jana.

KUNDI E

  • ZAMBIA 3
  • TANZANIA 3
  • MOROCCO 3
  • NIGER 3
  • CONGO 3
  • ERITREA 3

Makala Nyingine

More in FIFA World Cup