Klabu ya Young Africans kupitia kwa mjumbe wa kamati ya utendaji ya klabu hiyo Alex Ngai amesema tangu watue nchini Algeria hawajafanya mazoezi kuelekea mchezo wa kesho wa Ligi ya mabingwa Barani Afrika dhidi ya klabu ya CR Belouizdad.
Ngai ameeleza chanzo cha timu hiyo kutokufanya mazoezi ni kutokana na mizigo yao yote waliyoenda nayo kubaki kwenye ndege jambo ambalo limewapa usumbufu mkubwa, huku mizigo baadhi ikiwasili na kundi la pili la wachezaji waliokuwa kwenye majukumu ya timu ya Taifa.
Niwe muwazi tu Kuna changamoto kubwa imetokea ambayo haipaswi kutokea kwa timu ya mpira, mizigo yetu yote ambayo tulikuja nayo ilibaki kwenye ndege jambo ambalo limetupa usumbufu mkubwa.
Hatujafanya mazoezi toka tumekuja huku maana mizigo baadhi ilikuja jana na wachezaji waliowasili kutoka kwenye majukumu ya timu ya Taifa.
Lakini kwasasa mizigo yote imekamilika japo imetuletea usumbufu mkubwa sana ambapo karibia siku mbili hatujafanya mazoezi, leo tutafanya mazoezi ya mwisho kwenye uwanja ambao tutautumia kwenye mchezo huo.
Licha ya hivyo ila sisi hatujatoka mchezoni, tumeshakuwa wazoefu wa mashindano haya na michezo ya ugenini kwa hivyo sisi tutapambana kesho tupate matokeo”.
Alex Ngai, Mjumbe wa kamati ya Utendaji ya klabu ya Yanga.
Alex amesema pia hali ya hewa ni ya mvua tangu walipowasili nchini Algeria, mvua ambayo inanyesha kuanzia asubuhi hadi jioni lakini wao wanaendelea kujipanga na mchezo huo kikamilifu.
Tangu tulivyofika juzi na Jana tumeshinda na mvua tu, mvua inanyesha asubuhi, mchana na usiku na baridi ni la kutosha, hiyo ndio hali ya hewa ya huku ila haituondoi kwenye focus yetu ya mchezo wa kesho.
Alex Ngai, Mjumbe wa kamati ya Utendaji Young Africans.
Young Africans itacheza mchezo wake wa kwanza wa hatua ya makundi ya Ligi ya mabingwa Barani Africa dhidi ya CR Belouizdad siku ya kesho Ijumaa, November 24, majira ya saa nne usiku.