Chabab Riadhi Belouizdad wakijulikana kwa jina la Utani “The Chababists” ni klabu ya soka ya Nchini Algeria yenye umaarufu mkubwa, mashabiki wengi na mafanikio pia ya ndani lakini sio klabu yenye rekodi za kutisha kwenye michuano ya vilabu ya CAF.
Klabu hii ilianzishwa mwaka 1962 siku 10 tangu nchi ipate Uhuru na inautumia uwanka wa 20 August 1955, uwanja uliopo Belouizdad wenye uwezo wa kuingiza watazamaji 20,000 kama uwanja wao wa nyumbani.
Mahasimu wao wakubwa ni pamoja na Majirani zao MC Algers, USM Algiers pamoja na NA Hussein Dey.
Wakiwa wametwaa makombe ya ligi kuu mara 10 ikiwemo walilotwaa msimu uliopita(2022/23), Belouizdad wametwaa ubingwa huo mara 4 mfululizo tangu msimu wa 2019-2020 mpaka msimu jana. Ni miongoni mwa vilabu viliyotwaa ubingwa mara nyingi zaidi nchini Algeria wakiongizwa na JS Kabylie.
Belouizdad wamecheza Hatua ya Robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika(CAFCL) Kwa misimu mitatu mfululizo tangu 2020-2021 mpaka msimu jana ambao walitolewa na Mamelodi Sundowns kwa Jumla ya mabao 6-2. Wakifungwa nyumbani na ugenini na miamba hii ya ukanda wa COSAFA.
Kwa sasa timu ipo chini ya Kampuni inayojihusisha na Shughuli za Uwekezaji, MADAR HOLDING na ni miongoni mwa timu zinazowekeza hasa kwenye kuiboresha timu kila msimu kwenye ukanda wao wa UNAF.
Timu inaongozwa na Kocha Mbrazili Marcos Cesar Dias De Castro Paqueta aliyechukua nafasi ya Zoran Manojlovic tangu Septemba 23, 2021. Amefanikiwa kuwapa ubingwa wa ligi mara 2 mfululizo ikiwemo pia kuifikisha robo fainali mara 2 na msimu huu ameshaiingiza Hatua ya makundi. Pia ni muumini mkubwa wa soka la Kasi na mfumo wake pendwa ni 4-3-3 au 4-4-2 Diamond.
Belouizdad wanashika nafasi ya 3 kwenye msimamo wa Ligi kuu Algeria wakiwa na alama 12 nyuma ya Paradou(13) na Mahasimu wao MC Algers(15). Mchezo wao wa mwisho walicheza dhidi ya JS Kabylie na kushinda 1-0 Nyumbani.
Kutokana na sera ya soka nchini Algeria ya kulinda wachezaji wazawa, Belouizdad wana wachezaji watatu tu wa kigeni. Mkameruni Leonel Wemba, Mgambia Lamin Jallow na Mmali Mamadou Samake.
Hao Ndio CR Belouizdad, wapinzani wa Young Africans leo kwenye Dimba la 5 Juillet kuanzia majira ya saa 4 Usiku kwa saa za Afrika mashariki kwenye mchezo wa Ligi ya mabingwa Afrika, hatua ya Makundi.