Connect with us

CAF Champions League

YANGA YAPOTEANA ALGERIA

Wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Klabu ya Soka ya Yanga imeanza vibaya kampeni yake kwenye kundi D kwa kukubali kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa CR Belouizdad ya Algeria kwenye dimba la Stade Juillet 5 1962.

Licha ya kuwa nyumbani, Belouizdad walionyesha heshima kubwa kwa Yanga ambapo kocha Carlos Paqueta aliingia na mfumo wa 4-3-3 badala ya 4-4-2 Diamond anayotumiaga mara nyingi, akiwaanzisha nje Lamin Jallow na Leonel Wemba huku akijaza viungo watatu wakabaji na viungo wawili washambuliaji na mshambuliaji asili mmoja.

Yanga ni kama waliingia kwenye mtego huu na kuufungua uwanja mara kadhaa kujaribu kutafuta magoli. Belouizdad waliwajibu kwa mashambulizi ya kushtukiza ambapo mara hizo waliwakuta Yanga wako nje ya nidhamu yao ya ulinzi.

Kipindi cha kwanza Belouizdad waliwaadhibu vilivyo Yanga kila walipofanya makosa haya au kujichanganya wenyewe. Goli la Kwanza likifungwa na Abdelraouf Benguit akitumia uzembe wa safu ya ulinzi kutegeana kuuondosha mpira wa hatari langoni mwao.

Goli la Pili walitumia udhaifu wa viungo wa Yanga kuchelewa kurudi kutoka kwenye shambulizi na kukuta washambuliaji watatu wa Belouizdad dhidi ya Dickson Job na Ibrahim Bacca, pasi nzuri ya kukata ndani ya Oussama Darfalou ikamaliziwa kiurahisi na Abderrahman Meziane. Kila kitu kilionekana kuwa rahisi kwa Belouizdad hadi mapumziko.

Kipindi cha pili Mwalimu Gamondi aliamua kuufungua zaidi uwanja kwa kummtoa Mudathir Yahya na kumuingiza Clement Mzize na hivyo kubadili umbo kutoka 4-2-3-1 na kuwa 4-4-2, Mzize na Musonda wakicheza kama washambuliaji wawili na Pacome Zouzoua kutoka pembeni kabisa kama winga. Kwa dakika hizi Kitakwimu Yanga walimiliki mpira na kutengeneza nafasi kadhaa lakini hazikuzaa matunda.

Mwalimu Carlos Paqueta akafanya mabadiliko yake ya kiufundi na kuamua kumuingiza Wemba, Bakir na Guedioura ili kujaribu kupunguza kasi ya mashambulizi ya Yanga lakini bado moto ukawa ni ule ule hasa Gamondi alivyommtambulisha na Moloko kwenye Mchezo.

Alikuwa ni Lamin Jallow aliyeingia dakika ya 87 tu ya mchezo aliyekwenda kuutamatisha mchezo, tena kwa shambulizi la kujibu dakika ya 90+4 wakati Yanga wanatafuta chochote kitu. Pasi nzuri akitengewa na Meziane na kupiga shuti kali lililommshinda golikipa Metacha Mnata aliyeanza leo kuchukua nafasi ya Djigui Diarra.

Yanga wanapoteza mchezo wake wa kwanza wa kundi ugenini kwa mabao 3-0 wanarejea jijini Dar es Salaam kujiandaa na mchezo wao wa pili wa kundi hilo dhidi ya Al Ahly kwenye Dimba la Benjamin Mkapa tarehe 2/12/2023 kabla ya kuifuata Medeama wiki moja baadae.

KIKOSI KILICHOANZA

Metacha, Yao, Lomalisa, Job(c) , Bacca, Aucho, Mudathir, Maxi, Azizi Ki, Pacome na Musonda.

WACHEZAJI WA AKIBA

Mshery, Mwamnyeto, Kibabage, Mauya, Mkude, Sureboy, Moloko, Konkoni na Mzize.

MFUMO : 4-2-3-1

Makala Nyingine

More in CAF Champions League