Connect with us

NBC Premier League

MASSANZA: COASTAL UNION WANATAKA KIKI.

Coastal Union ya mkoani Tanga ipo mkoani Singida kwaajili ya kuikabili Singida Fountain Gate katika mchezo wa Ligi kuu kandanda Tanzania Bara unaotarajiwa kuchezwa leo saa 10:00 Jioni katika uwanja wa CCM Liti mkoani Singida.

Klabu ya Coastal Union jana imefanya mazoezi yake ya mwisho katika uwanja wa CCM Liti, uwanja ambao utatumika kwenye mchezo huo hii leo, wakati wakiendelea na mazoezi jana klabu hiyo ilichapisha taarifa ikieleza kuwa klabu ya Singida Fountain Gate ilivamia mazoezi yao kitu ambacho kwa mujibu wa kanuni haziruhusu.

Baada ya vurugu kadhaa kutokea mwenyekiti wa klabu ya Coastal Union ambaye pia ni mwenyekiti wa bodi ya Ligi na makamu wa pili wa Rais wa shirikisho la soka Tanzania Steven Mguto amesema Singida wamefanya makosa kwa mujibu wa kanuni na mtendaji mkuu wa bodi atalitolea taarifa.

Kanuni zipo wazi, ni juu ya Kamishna wa mechi kuripoti anavyoona na kamati italiangalia hilo, hapa lilipofika ni swala la mtendaji mkuu wa bodi kuweza kulitolea taarifa, vikao vitakaa na taarifa zitakuja kutolewa.

Kuna uhuni mwingi huku, watu wengine wanataka kuharibu chapa [Brand’ za timu zao, watu wanafanya kazi kubwa kuikuza chapa ya timu lakini wanakuja watu kuharibu tu, unajua kanuni kabisa zinakuelekeza kwamba siku moja kabla uwanja unatumiwa na mgeni.

Unapoongoza basi kuja kule na wachezaji mnataka kuja kufanya mazoezi sijui wanataka kuipaka matope timu yao ya Singida au namna gani sielewi, kwakweli uongozi wa Singida ni lazima uangalie watu wao wanaowatuma kufanya kazi.

Kwa camera zinavyoonyesha yule alishuka kwa shari akataka kwenda kupigana na mtu ambaye alikuwa anachukua video, katibu ndio mwendeshaji wa klabu yeye ndio anajua kama tutaandika barua au vipi.

Steven mguto, Mwenyekiti wa klabu ya Coastal Union.

Taarifa kutoka kwenye klabu ya Singida Fountain Gate kupitia kwa Afisa habari wa klabu hiyo Hussein Massanza amesema kilichotokea jana ni hali ya kukosa mawasiliano baina ya meneja wa uwanja na klabu ya Singida Fountain Gate, huku Coastal Union wameamua kulitumia swala hili kama ‘kiki’ ili wazungumzwe sana.

Kilichotokea jana ni hali ya mawasiliano ambayo hayakuwa yamekaa vizuri kwa pande zote mbili kwa maana ya Coastal Union walipaswa kufika saa 10:00 Jioni kwaajili ya kufanya maandalizi yao kama kanuni zinzvyoelekeza na tuliwapa ratiba hiyo.

Coastal walifika kweli saa kumi [10:00] lakini kutokana na dharura ambayo ilimpata meneja wetu wa uwanja alichelewa kufika hali iliyopelekea wageni wetu kuchelewa kuanza mazoezi.

Kwa bahati mbaya meneja hakuweza kuwasiliana kwa haraka na uongozi wa klabu hasa meneja wetu wa timu kumfahamisha kuhusiana na dharura hiyo na utaratibu wetu kama klabu timu ilitoka kambini nayo ikaja mazoezini kwasababu ratiba yetu ilikuwa ni jioni.

Kufika pale saa 11 ambao ndio muda Coastal walitakiwa waondoke katika uwanja wetu baada ya kumaliza programu yao ili sisi tuendelee na programu yetu, tukawakuta ndio kwanza wao wanaanza, sasa timu haikufanya mazoezi asubuhi na tayari imepanga ratiba zake ndio maana kukawa na huo msuguano.

Baada ya pale tulizungumza na wenzetu kuwaeleza kujaribu kufahamu kitu gani kilitokea ikafahamika ni sintofahamu hiyo ya mawasiliano lakini kwa bahati mbaya wenzetu walikuwa washaipeleka kwenye mitandao ya kijamii.

Nimefanya mawasiliano binafsi na viongozi wa Coastal Union kwa niaba ya klabu, kuhusiana na hali hii, lakini naona ni kama wenzetu wameing’ang’ania sana wanataka kuitumia kama kiki ya mechi hii muhimu.

Coastal ili wazungumziwe sana waliona hii ni fursa kwao kuing’ang’ania hivyo hivyo, ni kawaida kwenye mpira wa miguu wakati mwingine kutengeneza ‘hype’ ya mchezo, kutengeneza drama kwaajili ya kutengeneza mvuto wakufuatilie.

Singida tunafahamika vizuri hatujawahi kuwa na tabia hizi kwenye uwanja wetu wa nyumban, huwa tunakrimu watu wote wanaokuja kucheza hapa lakini pia hata ugenini hatujawahi kukutana na kashkash za namna hiyo.

Hussein Massanza, Afisa Habari na mawasiliano wa Singida Fountain Gate.

Singida Fountain Gate itashuka dimbani leo saa 10:00 Jioni kuikabili Coastal Union katika uwanja wa CCM Liti mkoani Singida ikiwa ni mwendelezo wa michezo ya Ligi kuu kandanda Tanzania Bara.

Makala Nyingine

More in NBC Premier League