Timo Werner kwenda Man Utd?! Erik ten Hag amemuongeza mchezaji wa zamani wa Chelsea katika orodha ya wachezaji anaotaka kuwasajili kuelekea katika dirisha dogo la usajili la mwezi Januari.
United tayari wamewasiliana na RB Leipzig kuhusu uwezekano wa kumnunua fowadi huyo wakati wa majira ya baridi, Sky Sport inaripoti kwamba hakuna ofa rasmi au mazungumzo kati ya timu hizo mbili hadi sasa. Real Madrid pia wamekuwa wakihusishwa nae lakini hawafikirii kumsajili kwa sasa.
Werner hayafurahii maisha akiwa na klabu yake ya RB Leipzig. Ameanza mechi mbili pekee kati ya nane za Ligi Kuu nchini Ujerumani (Bundesliga) ambazo ameshiriki msimu huu na kufunga mabao mawili. Hata hivyo, inasemekana kuwa yuko tayari kusubiri hadi dirisha la usajili la majira ya kiangazi kabla ya kufikiria kuondoka.
Werner alirejea RB Leipzig mwaka 2022 baada ya miaka miwili migumu akiwa Chelsea, ambapo alifunga mabao 23 katika michezo 89 katika mashindano yote. Alikuwa na mwanzo mzuri mara baada ya kurejea Ujerumani kwani alifunga mara tisa katika mechi 27 za Bundesliga, lakini amepoteza nafasi yake msimu huu.
United inaweza kuwa na wakati mgumu kumshawishi Werner kurejea katika Ligi Kuu kutokana na uzoefu wake, sambamba na anguko kubwa la kiwango chake wakati akiwa nchini Uingereza akiitumikia Chelsea na kuripotiwa nia yake ni kusalia na kupigania nafasi yake kwenye kikosi cha kwanza cha RB Leipzig kati ya sasa na mwisho wa msimu.