Klabu ya Young Africans imeanza safari leo alfajiri kuelekea nchini Ghana kwaajili ya mchezo wa tatu wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Medeama.
Yanga inasaka ushindi wake wa kwanza katika michuano hii baada ya kushindwa kupata ushindi katika michezo miwili iliyopita dhidi ya CR Belouizdad na Al Ahly.
Kuelekea katika mchezo huo Afisa habari na mawasiliano wa klabu ya Yanga, Ali Kamwe amesema mchezo huo utapigwa katika mji wa Khumasi na hautakuwa mchezo rahisi kutokana na aina ya wapinzani wake.
Tunaamini utakuwa mchezo mzuri, wenzetu sasa hivi wanajiamini sana, wameshinda mechi iliyopita dhidi ya CR Belouizdad.
Pengine wanaweza kutuchukulia sisi wachovu kwasababu tulifungwa na CR Belouizdad wao wakawafunga, tunataka watuchukulie hivyo mpaka tutakapofika uwanjani.
Bado wachezaji wanaimani kwamba, wanacho kitu cha kufanya kwenye hii champions League, na hilo ndilo linatufanya sisi viongozi, mashabiki na wanachama tuamini kwamba tuna nafasi ya kufanya vizuri kuanzia kwenye mchezo wa Medeama.
Haitakuwa mechi nyepesi, kwa jinsi nilivyowaona wachezaji, wako na ari kubwa na Morali kubwa na wanajiandaa kwaajili ya kwenda kutupa furaha wana Yanga.
Naamini kwa dua zao wana Yanga tutakuwa na mechi nzuri na tutaondoka Ghana tukiwa na matokeo mazuri.
Ali Kamwe, Afisa Habari wa klabu ya Yanga.
Yanga ipo mkiani mwa msimamo wa kundi D ikiwa na alama moja pekee iliyoipata katika mchezo dhidi ya Al Ahly waliyotoka sare ya 1-1 kwenye uwanja wa Taifa, Dar Es Salaam.
Huu ni mchezo mhimu zaidi kwa klabu ya Yanga ili kufufua matumaini ya kusonga kwenye hatua ya robo fainali ya Ligi ya mabingwa Barani Afrika.
Mchezo wa Medeama dhidi ya Yanga utapigwa katika Jiji la Khumasi nchini Ghana siku ya Ijumaa wiki hii.