Connect with us

NBC Premier League

MTIBWA SUGAR YACHAPIKA TENA

Mtibwa Sugar wameendelea kuwa na muendelezo wa matokeo mabaya wakikubali kichapo kingine wakifungwa 1-0 na Namungo kwenye mchezo wa Ligi Kuu soka Tanzania Bara, uliopigwa Kwenye dimba la Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi.

Namungo walikuwa wa kwanza kupata bao la kuongoza kupitia kwa Derrick Mukombozi dakika ya 8 tu ya mchezo akimalizia mpira wa pigo kubwa uliochongwa vizuri na Frank Domayo kisha mabeki wa Mtibwa Sugar kuzembea kuondosha mpira uliommkuta Mukombozi akiwa peke yake na kumalizia kiuwepesi.

Pengine ni uchanga tu wa timu ya Mtibwa Sugar ikiwa ni kikosi kilichosheheni vijana wengi kinasababisha kushindwa baadhi ya maamuzi hasa eneo la Ulinzi likiwa na vijana kama Toba Kutisha, Nickson Joseph na wengineo na eneo la kumalizia likiwa na wakongwe Matheo Anthony na Juma Liuzio. Lakini walijitahidi kucheza vizuri kipindi cha kwanza wakionana na kutengeneza mashambulizi na hata kuzuia kasi kubwa ya mashambulizi ya Namungo.

Wakicheza kwenye mfumo wa 4-2-3-1, Mtibwa walionekana kuwatumia Ladack Chasambi, Juma Nyangi na Kassim Haruna kupeleka mashambulizi kummsaidia Matheo Anthony na kujitahidi kujaribu kusawazisha lakini walionekana kuwa na papara na kushindwa kutumia vizuri nafasi.

Mpaka Mapumziko Namungo walikuwa mbele kwa bao 1-0.

Ukiachana na badiliko la kipindi cha kwanza la Namungo kumuingiza Hashim Manyanya nafasi ya majeruhi Hamadi Majimengi, timu zote ziliingia kipindi cha pili bila badiliko lolote.

Mtibwa Sugar walianza vizuri kipindi hiki cha pili wakiwa timu bora zaidi ya Namungo. Pasi fupi fupi lakini kasi walipokuwa wanakaribia eneo la penati la Namungo, ukikosekana tu utulivu.

Namungo hawakuwa nyuma kujibu mapigo na dakika ya 63 kama sio jitihada za mlinda mlango Toba Kutisha kuokoa shuti kali la Reliants Lusajo na kisha kwenda kugonga mwamba wa pembeni, basi Mtibwa wangetepeteshwa tena.

Kasi na utulivu wa Mtibwa Sugar ulimfanya Mwalimu Denis Kitambi kuimarisha safu yake ya ulinzi akiwapumzisha Frank Domayo nafasi yake akichukua James Mwashinga huku Erasto Nyoni akichukua nafasi ya Pius Buswita dakika ikiwa ya 71 ya mchezo.

Matheo Anthony anakosa nafasi ya wazi akipaisha kwa kichwa krosi nzuri ya Ladack Chasambi dakika ya 76.

Mpaka dakika ya 80 Mtibwa walikuwa siti ya mbele muda wote wa kipindi hiki. Vitalis Mayanga na Juma Liuzio waliingia kuingiza nguvu mpya kwenye safu ya ushambuliaji wakitoka Omary Suleiman na Matheo Anthony. Muda huo huo Namungo nao wanamuingiza Hassan Kabunda nafasi ya Jacob Massawe.

Licha ya Jitihada zote walizofanya Mtibwa kujaribu kupata chochote kitu kutoka kwenye mchezo huu bado waliambulia kichapo cha 5 mfululizo na kuendelea kujichimbia kaburi lao wenyewe.

Mpaka kipyenga cha mwisho cha muamuzi Hassan Mabena, Namungo 1-0 Mtibwa Sugar. Kwa matokeo haya Namungo anapanda mpaka nafasi ya 6 wakifikisha alama 17 wakiishusha JKT Tanzania huku Mtibwa Sugar akibaki nafasi yake ya 16 akiwa na alama 5 pekee.

Makala Nyingine

More in NBC Premier League