Asisat Oshoala, ni jina kubwa hivi sasa kwenye Ulimwengu wa soka na hasa la Wanawake. Akiwa na umri wa miaka 29, Oshoala amefanya mambo makubwa sana ikiwemo kuweka rekodi ya kutwaa tuzo ya CAF YA Mchezaji Bora wa Mwaka upande wa Wanawake mara 6.
Akitambulika kwa jina la utani la “The Female Seedorf” akifananishwa na mchezaji wa zamani wa Ajax, AC Milan na timu ya taifa ya Uholanzi, Clarence Seedorf, Oshoala alianza kucheza soka akitumikia nafasi ya ushambuliaji kwenye timu nyingi alizopita Lakini akitumika zaidi kama Kiungo mshambuliaji kwenye timu ya Taifa na hata Barcelona klabu yake ya sasa japo amesogezwa zaidi kama mshambuliaji.
Asisat amepita pia kwenye klabu ya Arsenal na Liverpool za wanawake kwenye nyakati tofauti lakini amejitengenezea zaidi jina lake FC Barcelona tangu ajiunge nayo mwaka 2019 akitokea Dalian Quanjian na kufunga mabao 83 katika michezo 89 aliyocheza na kumfanya kuwa miongoni mwa wachezaji bora kuwahi kutokea barani Afrika.
Asisat Oshoala ni mzaliwa wa huko Ikorodu, Nigeria akiwa ni mtoto wa Mzee Lamina Oshoala. Usiku wa kuamkia leo, amejiheshimisha yeye mwenyewe lakini pia soka la Nigeria na Afrika kiujumla. Kutoka kwenye maisha ya upambanaji kupitia vituo mbalimbali vya soka mpaka kutwaa tuzo ya 6 ya Mchezaji Bora Wa Mwaka kwa Wanawake ikiwa ni rekodi mpya kuwekwa. Anayefuatia kwa nyuma yake ni Mnigeria mwenzake Perpetua Nkwocha aliyetwaa tuzo hiyo mara 4.
Asisat Oshoala ametwaa tuzo hiyo mwaka 2014, 2016, 2017,2019,2022 na mwaka huu 2023 na ndiye mchezaji pekee kutwaa tuzo hii mara 3 mfululizo. Oshoala yupo kwenye dunia yake.
Unaikumbuka Ile Shangilia yake kwenye mchezo dhidi ya Australia kwenye World Cup walivyoshinda 3-2?