Ligi kuu ya soka ya wanawake Tanzania Bara Serengeti Lite Premier League imeanza kutimua vumbi rasmi hii leo kwa michezo mitatu kupigwa nchini.
Mabingwa watetezi JKT Queens walishuka dimbani hii leo kuikabili Bunda Queens katika mchezo uliomalizika kwa JKT Queens kuibuka na ushindi wa goli 4-0 wakiwa ugenini mkoani Mara kwenye uwanja wa Karume.
Magoli ya JKT Queens yamefungwa na Donisia Minja [2] na Winfrida Gerald [2].
Jijini Dar Es Salaam katika uwanja wa Azam Complex, Chamazi klabu ya Simba Queens ilikuwa mwenyeji wa Ceasia Queens katika mchezo uliomalizika kwa Simba Queens kuibuka na ushindi wa goli 5-0.
Magoli ya Simba Queens yalifungwa na Aisha Mnunka [3], Asha Djafar [1] na Mwanahamisi Omari [1].
Mchezo mwingine ulikuwa ukiihusisha Alliance Girls dhidi ya Geita Gold Queens mchezo uliomalizika kwa Alliance kuibuka na ushindi wa goli 2-1.
Magoli ya Alliance Girls yalifungwa na Nelly Kache [2] na goli la kufutia machozi kwa Geita Gold Queens lilifungwa na Thabea Aidano [1].
Ligi hiyo sasa inaongozwa na klabu ya Simba kwa tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa huku katika nafasi ya pili ikishikiliwa na JKT Queens, jumla ya magoli 12 yamefungwa leo.
Ligi hiyo itaendelea tena kesho kwa mchezo mmoja kuchezwa katika uwanja wa Jamhuri, Dodoma kwa kuikutanisha Baobab Queens dhidi ya Yanga Princess majira ya saa 10:00 Jioni.
ORODHA YA WAFUNGAJI WENYE MAGOLI MENGI.
- Aisha Mnunka [Simba Queens] [3].
- Nelly Kache [Alliance Girls] [2].
- Winfrida Gerald [JKT Queens] [2].
- Donisia Minja [JKT Queens] [2].
- Thabea Aidano [Geita Gold Queens] [1].
- Asha Djafar [Simba Queens] [1].
- Mwanahamis Omar [Simba Queens] [1].