Klabu ya soka ya Yanga wamefanikiwa kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Tabora United kwenye mchezo wa ligi kuu soka Tanzania Bara uliopigwa kwenye uwanja wa Jamuhuri, Dodoma huku Tabora United wakiwa nyumbani kiprotokali na kupunguza tofauti ya alama kati yao na Vinara wa ligi, Azam FC.
Pengine ni miongoni mwa mechi chache ambazo Yanga wamecheza na mfumo wa 4-4-2 msimu huu. Stephane Aziz Ki akicheza namba 10 sambamba na Kennedy Musonda(9) kwenye washambuliaji wawili ambapo Maxi Nzengeli na Jesus Moloko wakicheza kama mawinga huku Sureboya na Mudathir wakikamilisha safu ya Kiungo. Kutokuwepo kwa Pacome Zouzoua kwenye kikosi kinachoanza pamoja na Khalid Aucho kumeiua 4-2-3-1 leo hii.
Lakini yote haya hayakuzuia Yanga kucheza vizuri na kutengeneza nafasi za mabao. Wakitumia zaidi mapana ya Uwanja kupiga krosi lakini pia Mawinga kuingia ndani na kuongezeka kwenye safu ya Ushambuliaji kuliwapa wakati mgumu Safu ya ulinzi ya Tabora United chini ya nahodha Said Mbatty, Shaffih Maulid, Lulihoshi na Andy Bikoko.
Licha ya Tabora United kuonyesha kandanda safi lakini ni nyakati za ubora binafsi ndizo huamuaga matokeo wakati mwingine, Dakika ya 21, Stephane Azizi Ki aliitanguliza Yanga akifunga bao lake la 10 msimu huu.
Mpaka kwenda mapumziko Yanga walikuwa mbele kwa bao 1-0.
Kipindi cha pili kilirejea na kasi kama ya kipindi cha kwanza, timu zote zikionyesha kandanda safi huku mchezo ukiwa wazi kwa yoyote.
John Ben Nakibinge pamoja na Jackson Mbombo walicheza vizuri pembeni kwenye mfumo wao wa siku zote wa 4-4-2. Eric Okutu na Lumiere Banza walikuwa vema pia kwenye safu ya ushambuliaji lakini vita tamu ilikuwa katikati ya kiwanja bwana mdogo Najim Mussa akiendeleza ubora wake.
Yanga waliamua kuupoza mchezo huku wakionyesha pia kuridhika na matokeo na kuzidisha zaidi ulinzi wa bao hilo huku wakitengeneza nafasi chache. Hata hivyo golikipa John Noble alikuwa imara kuiongoza safu yake ya ulinzi.
Dakika zote 90 zikatamatika kwa Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0 buku ushindi huo ukiwafanya wafikishe alama 30, alama 1 tu nyuma ya vinara wa ligi, Azam.