Connect with us

Makala Nyingine

SIMBA YA SASA HAINA “VISHAZI HURU”

Kwa misimu takribani minne[4] mfululizo Klabu ya Soka ya Simba ilikuwa kwenye kilele cha mafanikio yao. Wakishinda takribani kila kitu kwenye Mashindano ya ndani lakini pia wakiwa tishio kwenye medani ya Kimataifa kati ya msimu wa 2017/18-2020/21.

Simba ni miongoni mwa vilabu vichache sana barani Afrika ambavyo vimeweza kucheza hatua ya Robo Fainali kwenye michuano yote ya Vilabu Afrika[CAFCL na CAFCC] kwa zaidi ya Mara 3 ndani ya Misimu 5. Ni rekodi ya aina yake.

Hawapo nafasi ya 7 kwa ubora Afrika[Kwa mujibu wa CAF 5 YEARS RANKING SYSTEM] au hata Kuwa na Sifa ya Kufuzu kucheza FIFA CLUB WORLD CUP 2025 kwa bahati mbaya, Simba wamefanya makubwa sana kwenye soka la vilabu Afrika ndani ya hii miaka 5 na ndio haswa kinachowatesa hivi sasa.

Hakuna msimu ambao Simba wameingia hatua ya makundi na wasifuzu hatua hiyo kuingia Robo Fainali, japo huishia hatua hiyo. Lakini alama walizojikusanyia na namna wanavyocheza kwenye michuano hii imewafanya wawe klabu bora kabisa ukanda huu wa CECAFA hadi kupewa heshima kuiwakilisha kanda hii miongoni mwa vilabu vyote kwenye michuano ya AFL iliyofanyika hivi karibuni, Simba ikitolewa na Al Ahly.

Haya yote yameifanya Simba kupewa heshima yake wanapokutana na timu za mataifa mengine nje ya nchi. Hakujawahi kuwa na mechi nyepesi Simba inapokutana na timu kwenye mashindano ya CAF. Wamejijengea ufalme wao huko. Haijalishi atakuwa kwenye hali gani. Ni Huu Mzimu wao wenyewe ndio unaowatesa.

Simba ya hivi karibuni imekuwa na nyakati mbaya sana kwakuwa haiwi timu inayoogopeka tena kwa mashindano ya ndani. Kila timu inajiamini ikicheza na Simba kwamba inaweza ikaambulia chochote ikijikaza.

  1. Wachezaji wake wanaonekana kuchoka. Waliokuwa bora misimu kadhaa iliyopita, ubora wao umeshuka na wengine wakichagizwa na umri wao. Uwezekano wa wao kuongezeka tena kiuwezo zaidi ya walipo hivi sasa ni mdogo sana. Kwa sasa wengi hawawezi kukupa mechi 5 mfululizo kwenye ubora ule ule na ni ngumu pia kutopata majeraha kwa msimu mzima.
  2. Kubwa zaidi ni kutokuwepo kwa wachezaji waamua mechi. Zipo nyakati nyepesi ambazo timu inaweza kucheza kawaida na ikapata matokeo lakini zipo nyakati ngumu ambazo unahitaji wakati wa mchezaji kuamua mechi(Individual Moment of Brilliance). Zilikuwepo nyakati ambazo mechi ikiwa ngumu kuna wachezaji zaidi ya watatu(3) walikuwa na uwezo wa kuibeba mechi yoyote begani na kulazimisha ushindi. Hiki kitu hakipo Simba sasa. Wachezaji wengi ni wanaotegemea “Link Up Plays” (Wachezaji Wategemezi) pekee. Timu ikibanwa, inabanika. Jean Baleke, Moses Phiri, John Bocco, Essomba Onana, Kibu Denis, Saidoo Hata Clatous Chama wote wanakosa ile hali ya kuamua mechi binafsi kwa sasa.
  3. Kuna baadhi ya wachezaji Viatu vya Simba ni vikubwa sana kwao na pengine kuna mengi makubwa yalitarajiwa kutoka kwao. Lakini soka ndivyo lilivyo, sio kila nyakati litakupa unachotarajia. Panapo maendeleo zipo pande huumia pia na haipaswi kuangaliwa nani ataumia zaidi na kufumba macho na kusonga mbele. Uthubutu huu kwa klabi ya Simba ni mdogo sana. Kwa rika walilo nalo Simba ni kuwa na wachezaji walio tayari na wenye ari hasa ya upambanaji. Sisemi Simba wana wachezaji wabovu, ila wengi hawapo tayari kukidhi mahitaji yao.

Ni hayo tu kwa sasa. Simba inateswa na Zimwi lake wenyewe. Kuna mengi wanapaswa kuyarekebisha kwa haraka kama kuna namna yoyote wanatazamia kufanya makubwa zaidi ya waliyofanya huko nyuma. Leo hii Simba wanapaswa kufahamu kuwa kutovuka hatua ya makundi ni anguko kwao.

Makala Nyingine

More in Makala Nyingine