Connect with us

Mapinduzi Cup

YANGA YAICHAPA JAMUS JIONI

Iliwabidi wasubiri mpaka dakika ya mwisho ya mchezo Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Jamus kwenye mchezo wa pili wa Kundi C kwa Yanga na kukaribia kufuzu hatua ya Robo Fainali.

Yanga walianza mchezo kwa kugawa nyakati na nafasi walizopo, wakicheza taratibu wakianza kujenga mashambulizi lakini punde mpira unapowafikia viungo washambuliaji watatu nyuma ya Mshambuliaji Clement Mzize kwa maana ya Jesus Moloko, Farid Mussa na Chrispin Ngushi kwenye mfumo wa 4-2-3-1 kasi iliongezeka na kuwaweka Jamus kwenye nyakati ngumu muda mwingi.

Timu ya Jamus ilikubali kuiheshimu Yanga wakicheza kwenye mfumo wa 5-3-2 huku wakicheza wakijilinda zaidi na kufanya mashambulizi ya kushitukiza. Wakiamini wamepata bao la utangulizi dakika ya 9 ya mchezo, lakini mfungaji alikuwa kwenye nafasi ya kuotea wakati anapokea pasi.

Licha ya kucheza kwa nidhamu, Jamus walikuwa wakifanya pia makosa mengi hasa kwenye eneo lao. Dakika ya 16 waliadhibiwa kwa makosa yao baada ya kusababisha faulo eneo hatarishi na mpira ukichongwa kiustadi kabisa na Farid Mussa kummshinda golikipa Marco Michael na kuitanguliza Yanga. Yanga 1-0 Jamus.

Yanga walidhani wamepata bao la 2 dakika ya 21 kupitia kwa Clement Mzize akiunganisha krosi safi ya Farid Mussa lakini mshika kibendera(muamuzi msaidizi) alikuwa na mawazo tofauti.

Dakika ya 35 Farid Mussa alishindwa kutumia makosa yaliyofanywa na mlinda lango wa timu ya Jamus, akipiga shuti lililokuwa hafifu na kwenda nje.

Jesus Moloko alipata nafasi pia ya kuandika bao kwa Yanga lakini shuti lake lilipanguliwa vema na Marko. Jamus waliendelea kuishi kiuhatarishi langoni mwao.

Jamus waliwashtukiza Yanga wakiwa bado wapo juu kwenye shambulizi. Mpira mrefu uliopigwa kutoka kwenye safu ya ulinzi, ulionekana kumshinda Mlinzi Kinda, Shaibu Mtita ambaye alipewa shinikizo na Yusuf Mulsar aliyeushinda mpira na kutoa pasi ya usaidizi kwa David Vincent ambaye naye hakufanya ajizi. Dakika ya 42, Yanga 1-1 Jamus.

Mapumziko timu zilienda vyumbani zikiwa sare 1-1

Jamus walionekana kubadilisha aina yao ya uchezaji ya tangu kipindi cha kwanza mwishoni. Wakijua hawawezi kupishana kiuwezo na wachezaji wa Yanga waliamua kucheza pasi chache kuelekea langoni kwa Yanga. Na mara kadhaa walifanikiwa wakiwakuta Yanga wako wachache kwenye eneo la ulinzi.

Yanga walimtambulisha Maxi Nzengeli na Skudu kwenye mchezo ili kuongeza kasi ya mchezo hasa eneo la umaliziaji. Lakini Jamus walikuwa imara mara hiii. Wakiwa watulivu kwenye eneo lao la ulinzi lakini wakiwa watulivu pia wakiwa na mpira.

Jamus wao waliendelea kucheza kwenye mpango wao huku wakiwaacha Yanga waumiliki mchezo kwa muda mwingi. Utulivu wao uliwafanya Yanga kushindwa maamuzi yao kiufasaha. Hawakuwa na mipango kabambe ya kushambulia Jamus lakini walikuwa na baadhi ya nyakati ambazo kilichokosekana ni utulivu tu kwenye eneo la mwisho.

Yanga walizidi kujenga mashambulizi huku wakitambulishwa mchezoni, Sheikhan na Nkane. Skudu alishuhudia mpira wake akiunganisha krosi kutoka kwa Dennis Nkane ukienda nje dakika ya 84 ya mchezo.

Haikuisha mpaka imeisha kwa Yanga, dakika za jioni kabisa, dakika ya 90+7, Nickson Kibabage akawainua Wananchi. Pasi nzuri kabisa kutoka kwa Clement Mzize, pengine kitendo chake bora kabisa cha mchezo mzima, ikaenda kwa Nickson Kibabage akitokea pembeni akapiga mpira kumshinda golikipa Marko na kuiandikia Yanga bao la 2 na la ushindi.

Dakika zote 90 zinatamatika, Yanga wanaibuka na alam zote 3. Kwenye mchezo ulioonekana kama unamalizika kwa sare ya 1-1, inaisha kwa ushindi wa 2-1 kwa Yanga na kusogelea karibu zaidi kucheza robo Fainali.

Nahodha, Laku wa Jamus alifanikiwa kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa Mechi huku Gift Fred wa Yanga akichaguliwa kuwa mchezaji mwenye nidhamu.

Makala Nyingine

More in Mapinduzi Cup