AC Milan iliyopo kwenye nafasi ya tatu [3] ya msimamo wa Ligi kuu nchini Italia, Jana ilikuwa na kibarua dhidi ya Udinese iliyopo nafasi ya 17 ya msimamo wa Ligi hiyo.
Mchezo huo ulimalizika kwa AC Milan ikiwa ugenini kuibuka na ushindi wa goli 3-2, ilikuwa ni miongoni mwa mechi bora sana kupigwa hapo jana na iligubikwa na mambo mengi sana ikiwemo ubaguzi.
Mlinda lango wa AC Milan Mike Maignan ni miongoni mwa wahanga wa ubaguzi huo kwenye mchezo wa jana ambapo anasema wakati akiwa langoni alikuwa anasikia mashabiki wanamuita nyani.
“Hatuwezi kucheza mpira kama hivi, tunapaswa kuacha, hatuwezi kukubali ubaguzi”.
“Mpira wa kwanza uliopigwa ukatoka nje kwetu nilisikia wanaimba nyani, sikusema chochote, mpira wa pili ulipotoka, wakafanya hivyo tena, nikaliita benchi na refa wa akiba wausimamishe mchezo”.
“Lazima kuwe na vikwazo vikali, kuongea tu hakuna maana yoyote, hatupaswi kabisa kukubali ubaguzi”.
“Wachezaji wenzangu walikuja kunikumbatia kama familia, tuko pamoja na siku zote wananiunga mkono”, Alizungumza Mike Maignan baada ya mchezo.
Swala la ubaguzi wa rangi Barani Ulaya bado linawakumba nyota wengi kwenye viwanja jambo ambalo linawafanya wafikirie kwenda kucheza soka mahali pengine.
Shirikisho la soka Duniani na mashirikisho ya soka Barani Ulaya yanaendelea kupinga vikali ubaguzi michezoni lakini bado mashabiki wanaendelea kufanya hivyo.
Maignan ameshauri kuwa wanapaswa kutengeneza sheria ngumu kwa mashabiki wanaofanya ubaguzi kwa makusudi ili kuikomesha tabia hiyo.