Connect with us

Taifa Stars

TAIFA STARS INAREJEA NCHINI KWA MAFUNGU.

Katibu mkuu wa wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo Gerson Msigwa amethibitisha kuwa kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania kimesafiri kwa mafungu kutoka nchini Ivory Coast kilipokuwa kikishiriki fainali za Mataifa ya Afrika [AFCON].

Msigwa amesema sababu ya timu ya Taifa ya Tanzania kusafiri kwa mafungu ni kukosa tiketi kwa kikosi kizima kilichokuwa Ivory Coast, hivyo ikapelekea baadhi ya wachezaji kusalia nchini Ivory Coast.

“Kuna changamoto kidogo ya usafiri, hatukufanikiwa kupata tiketi za timu nzima kwa mara Moja kwahiyo walioanza kuwasili nchini jana ni wachezaji na viongozi 15.

“Kuna baadhi yao watafika Leo wengine kesho. Nadhani kundi la mwisho watawasili kesho. Pia kuna wachezaji ambao wamerejea Moja kwa Moja kwenye nchi ambako timu zao wanazochezea”, Gerson Msigwa, Katibu Mkuu wizara ya Utamaduni,sanaa na Michezo.

Msigwa amesema kuwa kwasasa kama wizara wanaenda kuliwekea mkazo zaidi soka la vijana ili kutengeneza timu bora ya Taifa ya baadae, pia ameweka wazi namna ambavyo wanajipanga kwaajili ya WAFCON ambapo Tanzania itashiriki nchini Morocco.

“Hatupati matokeo mazuri hasa kwenye soka la wanaume watu wazima lakini tunafanya vizuri kwenye soka la wanawake”.

“Pamoja na kwamba tumeshiriki AFCON mwaka huu baada ya kufuzu kwa mara ya Tatu lakini kikubwa ni kwamba kwenye upande wa wanawake tumeweza pia kupata nafasi kushiriki AFCON ile ya wanawake kule Morocco”.

“Timu yetu ya wanawake inafanya vizuri na ni eneo jingine ambalo tumeliangalia kwa ukaribu lakini Moja ya mambo ambayo tunakwenda kuyatilia mkazo sana ni kwenye eneo la soka la vijana”, aliongeza Gerson Msigwa, Katibu Mkuu wizara ya Utamaduni,sanaa na Michezo.

Msigwa amesema kuwa wanapaswa kufanya uwekezaji kwenye soka zaidi hasa kwenye ujenzi wa miundombinu na mafunzo kwa wanamichezo.

“Changamoto yetu kubwa tulionayo bado tunahitaji kuwekeza zaidi kwenye soka au kwenye michezo kwa ujumla”.

“Tunahitaji kuwekeza kwenye miundombinu, mafunzo ya wanamichezo wetu (academy).

“Timu zetu nyingi ni watu wamejitafuta katika umri mkubwa wakaenda kwenye michezo wakaonekana wana vipaji wakafanya ndio maana wanafanya michezo kwa muda mfupi”, Aliongeza Gerson Msigwa.

Katibu wa Wizara ya Sanaa, Utamaduni na michezo ameweka wazi kuwa jana wamepokea ugeni kutoka nchini Ufaransa ambao ulikuwa na lengo la kuwapa mbinu ya namna gani ya kukuza soka la Tanzania ili ikiwezekana AFCON ya mwaka 2027 timu ya Taifa iwe bora zaidi.

“Jana tulikuwa na wadau wametoka Ufaransa wamekuja hapa nchini kutupatia mawazo ni namna gani tunaweza kutengeneza timu ya Taifa”.

“Tumewasikiliza wamefanya presentation yao. Tumewasikiliza na baada ya hapo tunakwenda kufanyia kazi. Tutakaloona tunaweza kulifanya kwa ajili ya kuimarisha zaidi timu ya Taifa Stars tunapoelekea AFCON 2027 ambapo tutakuwa sisi ndio wenyeji tutafanyia kazi”.

Tanzania imeondoshwa kwenye fainali za mataifa ya Afrika hatua ya makundi baada ya kuambulia alama mbili pekee ikimaliza nafasi ya mwisho ya msimamo.

Mwaka 2027 Tanzania inatarajiwa kuandaa fainali za mataifa ya Afrika kwa kushirikiana na nchi za Kenya pamoja na Uganda.

Makala Nyingine

More in Taifa Stars