Mshambuliaji mpya wa klabu ya Simba Fred Koublan amecheza mchezo wake wa kwanza dhidi ya Tembo inayoshiriki Ligi daraja la tatu nchini Tanzania kwenye michuano ya ASFC.
Fred hakufunga goli lolote licha ya kucheza dakika zote 90 za mchezo, nyota huyo ni miongoni mwa nyota wanaotarajiwa kufanya makubwa ndani ya kikosi hicho kutokana na takwimu bora alizokuwa nazo kwenye Ligi kuu soka nchini Zambia.
Baada ya mchezo wa ASFC kati ya Simba na Tembo mchambuzi wa soka nchini Gwamaka Francis amemfananisha nyota huyo na aliyekuwa mshambuliaji wa klabu ya Yanga raia wa Ghana Hafiz Konkoni, akisema aina ya uchezaji wao unafanana sana.
“Nimemtazama kwa umakini mshambuliaji mpya wa klabu ya Simba Fred Koublan ambaye amesajiliwa kwenye dirisha dogo la usajili kuziba nafasi ya Jean Baleke, ana sifa kama za aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga Hafidhi Konkoni”.
“Ni aina ya washambuliaji ambao wanasubiri mpira wa mwisho wa kufunga yani kutengenezewa, hawezi kwenda pembeni kutafuta mpira au kupokea mipira akiwa nje ya box la mpinzani”.
Fred hana kasi ya kukimbizana na mabeki wa timu pinzani, hivyo ni aina ya washambuliaji wanaohitaji sana msaada kwa viungo washambuliaji”, Alisema Gwamaka Francis.
Fred amesajiliwa dirisha dogo la mwezi January ili kuziba nafasi za nyota walioondolewa kikosini hapo kutokana na kutokuingia kwenye mfumo wa mwalimu Benchikha.
Simba iliibuka na ushindi wa goli 4-0 dhidi ya Tembo, na inatarajiwa kucheza mchezo wake wa kwanza wa Ligi wakitoka mapumziko dhidi ya Mashujaa Jumamosi hii kwenye uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.