Connect with us

NBC Premier League

AZAM YASHINDA, KAGERA YABANWA

Azam FC wameibuka na ushindi muhimu kwenye mbio za kuwania Ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara wa mabao 2-1 dhidi ya Geita Gold na kufikisha alama 35 kwenye nafasi ya 3, alama 1 tu nyuma ya Simba wanaoshika nafasi ya 2 wakiwa na alama 36.

Geita Gold walitangulia kupata bao dakika ya 40 kupitia kwa Tariq Seif Kiakala aliyepokea pasi ndefu kutoka kwa golikipa wake Costantine Deusdedith na yeye kuunganisha kwa shuti la mbali wakati golikipa Mohamed Mustapha akionekana kuwa nje ya goli lake.

Azam haikuwachukua muda kusawazisha bao hilo kwani dakika ya 44 ya mchezo, Prince Dube alitumia uzembe wa mlinzi Mwaita Gereza kutengeneza nafasi kwa Gybril Sillah aliyefunga kwa “tap in” tu mpira ambao ulishindwa kuokolewa na walinzi.

Dakika ya 83, alikuwa ni Iddy Selemani Nado aliyeamua alama 3 zinabaki Chamazi akiunganisha tena kwa “tap in” baada ya kona nzuri iliyopigwa na Cheikh Sidibe kushindwa kuokolewa na walinzi tena wa Geita Gold na mpira kumdondokea mfungaji.

Baada ya Dakika 90 za mchezo, Kocha wa Geita Gold, Denis Kitambi alikuwa na haya ya kusema

Kupoteza mchezo wa pili mfululizo na zaidi kuruhusu mabao ya ushindi dakika 10 za mwisho nadhani ni kitu ambacho tunapaswa kufanyia sana kazi, umakini dakika zote za mchezo muhimu sana. Hata hivyo angalau leo tumeweza kumiliki mpira na kucheza kidogo tofauti na mchezo uliopita. Nawapongeza wachezaji wangu kwa hilo lakini najipa pole kupoteza tena mchezo.

Kocha wa Azam, naye alikuwa na haya ya kusema

Tulijua lazima utakuwa mchezo mgumu, tumewatizama lakini pia wana wachezaji wazuri lakini sisi tulichojua ni kwamba lazima tushinde mchezo huu muhimu. Mbio za ubingwa ni ngumu sana msimu huu maana kila timu haitaki kupoteza alama hata 1 lakini ndio kinacholeta raha ya ligi, ushindani. Tumefurahi sana kupata alama hizi 3 leo.

Kwingineko kwenye dimba la Kaitaba huko Kagera, Mashujaa waliwabana mbavu wenyeji wao kwa sare ya 1-1.

Kagera Sugar walitangulia kupata bao kupitia kwa mshambuliaji wake Obrey Chirwa dakika ya 62 ya mchezo kabla ya Reliants Lusajo kuiandikia Mashujaa bao la kusawazisha dakika ya 76 na kufanya mchezo kumalizika kwa sare ya 1-1 licha ya timu zote kuonyesha kupambana kuibuka na ushindi.

Kwa Matokeo haya, Timu zite zinabaki kwenye nafasi zao, Kagera Sugar wakibakia nafasi ya 10 wakifikisha alama 18 huku alama 11 za Mashujaa zikiendelea kuwaweka nafasi ya 15 wazee wa Mapigo na Mwendo, alama 3 tu zaidi ya Mtibwa Sugar wanaoburuta mkia.

Makala Nyingine

More in NBC Premier League