Connect with us

NBC Premier League

YANGA YAREJEA KILELENI KIBABE

Yanga wamefanikiwa kurejea tena kileleni mwa Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 3-1 dhidi ya Namungo kwenye mchezo uliochezwa dimba la Majaliwa, Lindi na kufikisha alama 46 baada ya mechi 17.

Mabadiliko kwenye kikosi yaliwafanya Yanga wacheze kwa kasi ya chini kidogo kiuchezaji huku wakiwaruhusu Namungo kuwafikia muda mwingi golini kwao.

Dakika ya 15, Hassan Kabunda alipata nafasi ya kupiga shuti akiwa anatizamana na Metacha Mnata lakini shuti lake lilipanguliwa na kuwa kona.

Yanga walitumia zaidi mapana ya kiwanja huku upande wao wa kulia aliokuwa akicheza Yao Kouassi na Augustine Okrah ukitumika zaidi.

Dakika ya 28, Augustine Okrah alimsetia pasi nzuri Stephane Aziz Ki lakini shuti lake halikulenga lango.

Namungo walirudi tena langoni mwa Yanga kubisha hodi, Safari hii akiwa ni Emmanuel Asante aliyeruka juu kuunganisha kwa kichwa vizuri kona iliyochongwa na Hassan Kibailo.

Dakika ya 40, Salum Aboubakar alipata nafasi ya kupiga shuti akiwa nje ya 18 lakini Jonathan Nahimana alipangua.

Mapumziko timu zote zilitoka kwa suluhu ya 0-0.

Kipindi cha Pili lakini walirejea kwa kasi zaidi ya kipindi cha kwanza. Dakika ya 47 walipata nafasi ya kupata bao lakini Nahimana kwa mara nyingine akawa mwokozi.

Dakika ya 54, Yanga walipata bao la kuongoza kupitia kwa yule yule Mudathir Yahya aliyewaumiza kwenye mchezo wa kwanza, akipokea pasi kutoka kwa Stephane Aziz Ki kisha akakandamiza msumari uliomshinda Nahimana.

Yanga walirudi tena kwa kasi kwenye lango la Namungo, Dakika ya 58, Clement Mzize alitumia makosa ya mlinzi Derrick Mukombozi aliyekuwa akichezea mpira kwenye eneo lao akaunasa Mzize aliyemchungulia tu Nahimana amekaaje na yeye kuukwamisha pembeni kabisa mwa lango lake. 2-0 Yanga.

Stephane Aziz Ki alifunga bao lake la 11 msimu huu na la 3 kwa Yanga kwenye mchezo huu dakika ya 62 akipokea pasi murua kutoka kwa Yao Kouassi Attohoula akapiga shuti kali lililomshinda tena Nahimana. 3-0 Yanga.

Dakika ya 68 Namungo walikosa nafasi ya wazi ya kurudisha goli kupitia kwa Pius Buswita aliyejikuta peke yake na lango lakini akaweka mpira nje.

Namungo walirudisha goli 1 dakika ya 71 kupitia kwa krosi iliyochongwa na Emmanuel Charles kumbabatiza Ibrahim Bacca na kutinga kimiani. 3-1.

Namungo walifanya mabadiliko akiingia James Mwashinga, Hamadi Majimengi na Kelvin Sabato nafasi za Hamisi Nyenye, Pius Buswita na Meddie Kagere. Huku Yanga wakimuingiza Shekhan Ibrahim nafasi ya Augustine Okrah.

Dakika ya 85 Yanga walifanya mabadiliko mengine kuwaingiza Jonas Mkude na Bakari Mwamnyeto nafasi za Mudathir Yahya na Maxi Nzengeli. Huku Hashim Manyanya akiwa uwanjani kumpokea Hassan Kabunda upande wa Namungo.

Licha ya Namungo kucheza vizuri dakika za mwisho za mchezo lakini hawakuwa makini kwenye kuzitumia nafasi zao hasa Ibrahim Mkoko ambaye alipata nafasi nyingi za wazi lakini alishindwa kuzitumia.

Dakika zote 90 zikatamatika kwa Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 3-1.

Makala Nyingine

More in NBC Premier League